Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia na ukatili katika mzozo wa Syria vimefikia viwango vya kupindukia: Ban

Ghasia na ukatili katika mzozo wa Syria vimefikia viwango vya kupindukia: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amesema mzozo wa Syria, ambao sasa umeingia mwezi wa 21, umefikia viwango vipya vya kushangaza vya ukatili na machafuko.

Bwana Ban amesema hayo wakati akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo pia limehutubiwa na Mwakilishi maalum wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na jumuiya ya nchi za Kiarabu, Lakhdar Brahimi. Bwana Ban amesema, serikali ya Syria imeongeza moto katika kampeni yake ya kuyafyeka maeneo yote ya upinzani, na kuongeza mashambulizi yake ya angani na mizinga, huku upinzani ukijibu.

Bwana Ban amesema ingawa Umoja wa Mataifa hauwezi kuthibitisha kihuru takwimu zilizopo sasa, inakadiriwa kuwa hadi watu 40, 000 wameuawa. Ukiukaji wa haki za binadamu unatekelezwa kwa viwango vya kupindukia na pande zote katika mzozo.

Ameelezea huzuni yake na kulaani vikali mauaji ya kikatili ya raia kila siku, akisema kwamba ukatili dhidi ya ubinadamu ni lazima ukomeshwe, na wahusika kuwajibika.