Zaidi ya nchi 60 zinajihusisha na mkakati wa nishati endelevu kwa wote:Ban

24 Septemba 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, amesema kuwa tangu kuzinduliwa kwa mkakati wa nishati endelevu kwa wote mwaka uliopita, zaidi ya nchi 60 zinazoendelea zimejiunga kwenye jitihada za kuuendeleza, huku nyingine zikiwa zinajiunga nao.

Bwana Ban amesema kuwa kampuni za biashara zimejitolea kuufadhili mkakati huu kwa zaidi ya dola bilioni 50 za kimarekani, huku serikali na wadau wengine zikiwemo benki za kimataifa, zikiahidi mabilioni ya fedha zaidi.

Amesema imekuwa ni safari ndefu kufikia nafasi hii, na bado kuna mwendo mrefu mbeleni, ili kufikia upatikanaji wa nishati ya kisasa kwa wote ifikapo mwaka 2030. Ameongeza kuwa kasi ya kuboresha matumizi ya nishati inatakiwa kuongezwa maradufu kote duniani ili kuyafikia malengo yalowekwa ifikapo mwaka 2030.