Ban ana matumaini kuwa Baraza la Usalama litakuwa na Sauti Moja kuhusu Mzozo wa Syria
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ameelezea matumaini yake kuwa Baraza la Usalama, ambalo Uchina ni mwanachama wake wa kudumu, litaendelea mazungumzo yake kuhusu Syria.
Akikutana na rais Hu Jintao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uchina mjini Beijing leo, Bwana Ban amesema anatumai kuwa, kama suala la dharura, Baraza la Usalama litaungana kwa ari moja ili kusaidia kukomesha umwagaji damu na kuwapa raia wa Syria nafasi ya kuanza mazungumzo yatakayopelekea kuunda serikali ya mpito.
Wakati wa mkutano huo, ameishukuru Uchina kwa nafasi yake ya uongozi ushiriki kikamilifu katika Umoja wa Mataifa. Ameelezea pia umuhimu wa Uchina katika kuimarisha amani na usalama duniani, pamoja na kuchagiza maendeleo endelevu.