Skip to main content

Ban awasihi viongozi Kote Duniani Kutumia Vyombo vya Habari vya Kijamii

Ban awasihi viongozi Kote Duniani Kutumia Vyombo vya Habari vya Kijamii

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, leo ametoa wito kwa viongozi kote duniani kutumia vyombo vya habari vya kijamii kama vile Twitter na Facebook mara kwa mara, hata zaidi ya jinsi anavyofanya yeye. Bwana Ban ambaye yuko ziarani Uchina, amesema amekuwa akiwasiliana mara kwa mara kupitia njia hii, ili kutoa ujumbe kwa dunia nzima, na kutoa mfano wa kuhusika kwake hivi karibuni kwenye Google Hangout, ambayo amesema aliitumia kuwafikia mamilioni ya watu na ujumbe wake.

Amesema kuwa tovuti imeubadilisha ulimwengu mzima kwa njia nyingi, na kwamba ni njia ya ubunifu na iliyo bora ya kuwafikia watu na kuunganishwa nao. Amesema Umoja wa Mataifa una malengo na miradi muhimu, na kwamba ni vizuri kuwafikia watu kote ulimwenguni ili kushirikiana nao kuhusu malengo na miradi hii. Amesema kuna habari nyingi muhimu ambazo zinastahili kuwafikia watu wengi kwa muda mrefu, na kwamba vyombo vya habari vya kijamii vinaweza kusaidia kufanya hivyo:

‘Natumai kwamba viongozi wa kimataifa watavitumia vyombo hivi mara kwa mara. Wana nguvu na ubunifu. Huu ubunifu na nguvu vinastahili kuletwa pamoja na kutumiwa vyema, na hiyo ndiyo kazi ya vyombo hvi vya habari vya kijamii. Kama katibu Mkuu, nimeiga mengi, kwamba si tu Umoja wa Mataifa, wala Katibu Mkuu pekee, bali viongozi wa kimataifa pia. Wana wajibu, kuzungumza na kujadili na watu wengi ambao wasingeunganishwa nao bila vyombo vya habari vya kijamii. Ni lazima tuvitumie kwa manufaa ya ulimwengu wetu wa sasa.”