Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Rio+20 ni fursa muhimu kwa kizazi hiki:Ban

Mkutano wa Rio+20 ni fursa muhimu kwa kizazi hiki:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, amesema mkutano wa kimataifa wa Rio+ 20 ni fursa ya kipekee katika kizazi kizima ya kupiga hatua ya kufikia uchumi endelevu wa siku zijazo.

Bwana Ban ameongeza kuwa mkutano huo unaweza kusaidia kujenga ulimwengu wenye usawa, ambao ni wenye ufanisi mkubwa zaidi, na wenye kujumuisha wote, pamoja na kulinda mazingira.

Amesema katika mazungumzo ya wiki ilopita, hatua muhimu zilipigwa, na kwamba viongozi wanaokwenda kwenye mkutano wa Rio+20 wanahitajika kuyafanya maswala yatakayojadiliwa kuwa hoja zao binafsi.

Bwana Ban amesema kuwa ulimwengu wa sasa ni wenye uchumi unaoyumbayumba, usokuwa na usawa na wenye hali ya mazingira inayozorota.

Hivyo basi, anatarajia kuwa mkutano wa Rio utakuwa na matokeo ambayo yatabadili hali ya maisha ya watu kote ulimwenguni, kwa kutoa jawabu kwa changamoto muhimu, kama vile kuongeza nafasi za kazi na ulinzi wa kijamii, nishati, uchukuzi na usalama wa chakula.