Maendeleo ya malengo ya Milenia ya kupatikana kwa maji yatimizwa

6 Machi 2012

Ulimwengu umetimiza lengo la maendeleo ya milenia ya kupunguza kwa nusu idadi ya watu wasio na maji safi ya kunywa.

Hii ni kwa mujibu wa shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF na lile la afya duniani WHO.

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba kwa muda wa miaka kumi iliyopita zaidi ya watu bilioni mbili walipata maji safi ya kunywa na huduma zingine za kuhakikisha upatikanaji wa maji kama vile mabomba ya maji na visima.

Ulimwenguni kote asilimia ya watu 89 ya watu wote bilioni 6.1 walio duniani kwa sasa wanapata maji ikiwa ni asilimia moja zaidi ya ile ya malengo ya milenia.

Hata hivyo ripoti hiyo inasema kwamba nchi nyingi zilizo kusini mwa jangwa la sahara zimebaki nyuma lakini kuna mafanikio kadhaa  nchini Malawi, Burkina Faso , Ghana , Namibia na Gambia.