Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DR. Congo inaweza kuendelea sana ikitumia misitu yake vyema:UNEP

DR. Congo inaweza kuendelea sana ikitumia misitu yake vyema:UNEP

Utafiti uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP unasema Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaweza kuwa na maendeleo makubwa sana barani Afrika endapo itapunguza shinikizo na kushughulikia haraka matatizo yanayoikabili sekta yake ya mali asili.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ndio yenye nusu ya misitu ya bara la Afrika, ina vyanzo vikubwa vya maji na madini ya matrilioni ya dola. Utafiti huo ambao ni wa kutathimini hali ya Congo baada ya vita umeeleza umuhimu wa mali asili ya Congo kitaifa na kimataifa. Lakini hata hivyo umeonya juu ya ongezeko la ukataji miti, mauaji ya viumbe vilivyo katika hatari ya kutoweka, uchafuzi wa mazingira, na mmomonyoko wa udongo unaosababishwa na uchimbaji wa madini na matatizo ya upungufu wa maji yaliyoathiri watu milioni 51. Utafiri huo uliotolewa leo mjini Kinshasa umesema matatizo haya yanahitaji suluhu ya haraka.