Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azishauri serikali kuunda sera za huduma kwa familia

Ban azishauri serikali kuunda sera za huduma kwa familia

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki moon amesema kuwa serikali zinahitaji kubuni sera ili kuhakikisha kuwa familia maskini zimepata huduma zinazotakikana ili kuboresha maisha ya baadaye kwa watoto wao.

Akiongea wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya familia inayoadhimishwa kila tarehe 15 mwezi Mei Ban amesema kuwa ugumu zinazopitia familia nyingi huenda ukawa athari za muda mrefu na vigumu kujikwamua kutoka kwenye umaskini.

Ban amesema kuwa kuna familia zilizo kwenye aina nyingi ya hatari zikiwemo familia kubwa na zilizo na mzazi mmoja ambapo wanaotegemewa hawana ajira au wanasumbuliwa na magonjwa.

Ban ameongeza kuwa kuboreshwa kwa sera hizi ambazo zinaweza pia kuboresha lishe na elimu kwa watoto kutoka kwa familia hizi kutasaidia kumaliza umaskini uliokithiri kwa vizazi vingi.