Fursa inahitajika kuwasaidia Wasomali walioathirika na ukame:UM

22 Machi 2011

Mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kibinadamu nchini Somalia Mark Bowden ametoa wito wa kuwepo na fursa ya kuweza kuwasaidia Wasomali wanaokabiliwa na ukame na machafuko yanayoendelea hasa katikati na Kusini mwa Somalia.

Amesema wakati dunia leo ikiadhimisha siku ya maji duniani bidhaa ambayo ni muhimu kwa uhai, hakuna mahali ambapo yahahitajika zaidi kuliko Somalia, ambako watu wengi wanateseka , na kuhangaika kupata maji kwa ajili ya maisha yao, ya mifugo yao na ya mazao pia.

Amesema ukosefu wa mvua za masika umesababisha watu milioni 2.4 sawa na asilimia 32 ya Wasomali wote kuhitaji msaada. Amesema bei za vyakula zimepanda, wengi hawapati chakula na matatizo ya utapia mlo yameongezeka.

Ameongeza kuwa hofu yake ni athari za ukame uliokithiri kwa wanawake, watoto na jamii nzima ambapo watu 50,000 wameshakimbia makazi yao. Bowden amesema na hali inakuwa mbaya zaidi ikichangiwa na vita vinavyoendelea nchini humo kwa miongo miwili sasa.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter