Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha matokeo rasmi ya kura ya maoni Sudan

Ban akaribisha matokeo rasmi ya kura ya maoni Sudan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akaribisha matokeo rasmi na ya mwisho ya kura ya maoni ya endapo watu wa Sudan Kusini wajitenge na kuwa taifa huru ama la.

Matokeo hayo yanaonyesha kwa asilimia 98.83 ya wapiga kura zote wamechagua kujitenga na kuwa taifa huru jambo ambalo Ban amesema ni matokeo ya matakwa ya walio wengi Sudan Kusini. Ameongeza kuwa kufanyika kwa amani na utulivu kwa kura hiyo ni mafanikio makubwa kwa Wasudan wote.

Katibu Mkuu amewapongeza wadau wa makubaliano ya amani ya CPA, serikali ya Sudan inayoongozwa na Rais ,Omar Hassan Al Bashir, na serikali ya Sudan Kusini inayoongozwa na Rais Salva Kiir Mayardit, kwa kutekeleza ahadi zao za kuhakikisha amani na usalama wakati wa mchakato mzima wa kura ya maoni.

Ban amewataka wadau wote wa makubaliano ya CPA serikali za Kaskazini na KusiniThe kuendelea mchakato huo wa mafanikio ya kura ya maoni ili kufikia muafaka wa mipango ya baada ya kura ya maoni ikiwemo suala la Abyei, kwa ushirikiano.

Ban ameitaka jumuiya ya kimataifa kuwasaidia Wasudan kuelekea kwenye utulivu wa kudumu na maendeleo na amerejea nia ya Umoja wa Mataifa ya kuhakikisha inaendelea kutoa msaada kwa Sudan na kwa wadau wa maafikiano ya CPA