Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji wana mchango mkubwa katika uchumi wa kimataifa: Ban

Wahamiaji wana mchango mkubwa katika uchumi wa kimataifa: Ban

Wakati kwa wengi uhamiaji unaonekana kama ni jambo zuri na uzoefu wenye tija, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kwa wengine wengi wanaendelea vitendo vya ukiuakaji wa haki za binadamu, mauaji ya kuwalenga wageni na unyonyaji dhidi ya wahamiaji.

Katika ujumbe maalumu kwa siku ya kimataifa ya wahamiaji iliyoadhimishwa jana Desemba 18 Ban amezitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuridhia mkataba wa kuwalinda wafanyakazi wageni na familia zao. Ikikadiriwa kuwa na wahamiaji wa kimataifa milioni 214 amesema ni muhimu kukumbuka jukumu kubwa linalofanywa na wahamiaji hao katika kuimarisha uchumi wa kimataifa.

Ameongeza kuwa wahamiaji pia wanaongeza nakshi katika jamii kwa kuleta tamaduni mbalimbali, ujuzi na kubadilishana teknolojia, na kuongeza uwiano katika masuala ya idadi ya watu na umri wa kuzeeka katika jamii hizo. Amesisitiza haja ya kulinda haki zote za wahamiaji na utu wao, hata wale wasio halali kutokana na sheria za kimataifa.