Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban amezitaka nchi zinazoendelea kukusanya rasilimali kupambana na umasikini

Ban amezitaka nchi zinazoendelea kukusanya rasilimali kupambana na umasikini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo amezitaka nchi zinazoendelea kutumia ujuzi na rasilimali walizonazo kuharakisha mchakato uliokubalika kimataifa kufikia malengo ya kupunguza umasikini ifikapo 2015.

Amesema nchi zinazoendelea ambazo zinatumia ujuzi, kubadilishana mawazo na kuratibu mipango vizuri wanaweza kupata faida kubwa kuliko ambayo wangeweza kupata bila kufanya hivyo. Ban ameyasema hayo katika ujumbe maalumu kuadhimisha siku ya Umoja wa Mataifa ya ushirikiano wa Kusini-Kusini.

Amesema tamasha la kimataifa la hivi karibuni kuhusu ushirikiano wa Kusini-Kusini mjini Geneva limeonyesha kwamba ushirikiano wa namna hiyo unaweza kuimarisha na kusaidia sana katika masuala ya kazi bora, usalama wa chakula, mabadiliko ya hali ya hewa , afya na elimu.

Ban pia amechagiza umuhimu wa ushirikiano huo katika kufikia malengo ya maendeleo ya milenia ambayo yanampango wa kupunguza umasikini na njaa, vifo vya kina mama na watoto na ukosefu wa huduma za afya na elimu ifikapo 2015.Ameongeza kuwa katika muongo mmoja tangu kuanzishwa mkakati wa malengo ya milenia nchi nyingi zimepiga hatua katika kuandikisha watoto wanaoanza shule, kupunguza vifo vya watoto wachanga, kuimarisha hali ya kupata maji safi na salama na juhudi za kupambana na malaria, HIV/AIDS na maradhi mengine.

Amesisitiza ingawa kuna mafanikio hayo lakini bado watu bilioni 1.7 katika nchi 104 bado hawawezi kupata huduma muhimu na za lazima katika maisha ya kila siku , amesema kwa kulitambua hilo ushirikiano wa Kusini-Kusini ni muhimu sana kuyakabili matatizo hayo. Amesema katika siku hii ya Umoja wa Mataifa tuongeze mshikamano na umoja wetu kuhusu malengo ya maendeleo ya milenia kwani 2015 inakaribia, tuweze kuwa na amani, matarajio na maisha bora kwa wote.