Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maji ni uhai na ni haki ya binadamu bila maji hakuna maisha:Ban

Maji ni uhai na ni haki ya binadamu bila maji hakuna maisha:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema maji sio tuu ni ya lazima katika maisha bali ni haki ya binadamu, kwani bila maji hakuna maisha.

Ban ameyasema hayo kwenye mkutano maalumu kwenye baraza la Umoja wa Mataifa mjini New York wenye lengo la kushughulikia chanmgamoto za kimataifa za maji na usafi. Ban amesema ingawa bidhaa hiyo ni muhimu sana lakini bado mamilioni ya watu hawawezi kupata maji safi na salama.

Inakadiriwa kuwa watu bilioni 2.6 duniani hawana vifaa ya usafi kama vyoo, mazingira ambayo yanaongeza tishio la magonjwa na vifo na kuzidisha hali ya umasikini. Ban ametoa wito kwa dunia kuongeza juhudi, amesema tuko katika njia inayotakiwa ya kufikia malengo ya maji kwa wote, lakini ripoti zote zinaonyesha kwamba lengo la milenia la usafi liko nje ya msitari, na hasa katika maeneo ya vijijini.

Amesema ni lazima tufanye kazi kwa haraka ili kuhakikisha kila mtu duniani anaweza kupata maji safi na salama kila siku na ili kufanikisha hilo mabadiliko makubwa yanahitajika katika sera za afya ya jamii na miundombinu kufanikisha mambo ya usafi.