Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa UM wa malengo ya milenia unaendelea

Mkutano wa UM wa malengo ya milenia unaendelea

Nchi mbalimbali zimeendelea kutoa tathimini ya hatua zake katika malengo ya maendeleo ya milenia kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini New York ambao leo umeingia siku ya pili.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amesema licha ya shinikizo na vikwazo kutoka nchi za Magharibi nchi yake imepiga hatua kubwa katika kufikia malengo hayo. Rais Mugabe amesema nchi yake inatoa msisitizo kwa malengo namba moja tatu na sita ambayo yanahusiana na kutokomeza njaa, kuwawezesha wanawake na kukabiliana na maradhi .

(SAUTI RAIS MUGABE)

Mugabe amesema pia wamepiga hatua kubwa katika uandikishaji wa watoto katika shule za msingi na kupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi mapya ya ukimwi. Ila amesema bado wana changamoto kubwa kwa sababu ya vikwazo ilivyowekewa nchi hiyo japo wana imani kuwa wanaweza kutimiza malengo ya milenia.

Kwa upande wake Malawi imesema ina uhakika wa kutimiza malengo ya milenia ifikapo 2015, na hasa katika kuhakikisha imetokomeza umasikini, njaa, magonjwa na masomo ya elimu ya msingi. Jason Nyakundi anaarifu.

(RIPOTI YA JASON NYAKUNDI)

Akihutubia mkutano mkuu wa umoja wa mataifa kuhusu malengo ya milenia rais Mutharika amesema kuwa malengo matano kati ya malengo yote manane yatatimizwa hata kabla ya mwaka 2015. Rais Mutharika ameongeza kuwa malengo matatu yakiwemo ya elimu , usawa wa kijinsia na kupunguza vifo vya watoto yanahitaji jitihada zaidi.