Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za dharura zimetangazwa Chile kufuatia tetemeko la ardhi

Hatua za dharura zimetangazwa Chile kufuatia tetemeko la ardhi

Rais wa Chile Michelle Bachelete ametangaza hatua za dharura ili kukabiliana na uharibifu uliofanywa na tetemeko kubwa la ardhi siku ya Jumamosi .

Tetemeko hilo lililokuwa na ukubwa wa 8.8 vipimo vya rishita, ni moja ya matetemeko makubwa kuwahi kutokea nchi humo na limelikumba eneo la kati ya Chile, na kukatili maisha ya watu 700.

Vikosi vya jeshi vimepelekwa katika eneo lililoathirika ili kusaidia shughuli za uokozi na kuzuia uporaji. Rais Bachelet ameahidi msaada wa haraka wa chakula, maji na malazi kwa maelfu ya watu walioachwa bila makazi ambao kwa sasa wanalala mitaani.

Ofisi ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon imesema inafuatilia kwa karibu maendeleo ya Chile na pia hatari ya kutokea tsunami katika ukanda wa Pasific. Hata hivyo onyo la tsunami Pasific limeondolewa ingawa Japan bado imeweka kiwango kidogo cha tahadhari na imewahamisha watu 32,000 kutoka eneo la hatari.