Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahisani wahimizwa na UNCTAD kutekeleza ahadi za kuimarisha kilimo Afrika

Wahisani wahimizwa na UNCTAD kutekeleza ahadi za kuimarisha kilimo Afrika

Kwenye kikao cha Bodi la Utawala la Shirika la UM juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD) kilichofanyika Ijumanne Geneva kuzingatia mzozo wa chakula katika Afrika, wahisani wa kimataifa walihimizwa kutekeleza haraka ahadi walizotoa siku za nyuma kuimarisha kilimo bora barani humo.

UNCTAD inaamini maendeleo ya kilimo ndio yenye ufunguo utakaosaidia bara la Afrika kupata akiba maridhawa ya chakula itakayokidhi mahitaji ya umma.  Shirika la UNCTAD linakadiria watu milioni 300 ziada katika Afrika - sawa na thuluthi moja ya idadi ya watu - hukabiliwa na tatizo la njaa sugu kila siku. Mataifa 21 ya Afrika sasa hivi hutegemea mahitaji ya chakula kutoka vyakula viingizwavyo nchini mwao kutoka nje, hali ambayo huathiri sana umma kwa sababu ya bei za kigeugeu katika soko la kimataifa, hususan zile bei za bidhaa ya vyakula vikuu kama mchele, ngano, mahindi na vile vile bei ghali ya mafuta ya kupikia, ambayo watu wa kawaida hawazimudu. Mkurugenzi Mkuu wa UNCTAD, Supachai Panitchpakdi aliwakumbusha wajumbe wa Bodi la Utawala ya kwamba bara la Afrika, tangu awali, lilishambuliwa na mizozo kadha wa kadha mengine, ambayo chanzo chake kinatoka nje ya eneo, migogoro ilioathiri sana hali ya uchumi na jamii. Aliifananisha hali hiyo sawa na "mwaathirika mtazamaji asiye hatia" anayedhurika na mizozo ya wengine iliojumlisha uhaba wa chakula, miporomoko ya fedha na bei ya juu ya nishati. Alihadharisha Mkuu wa UNCTAD dhidi ya tabia karaha ya nchi wanachama, kutoyapa umuhimu unaostahiki mahitaji ya umma wa Afrika, katika wakati ambao huonnekana wamekakamaa kukabiliana na matatizo ya fedha kwenye soko la kimataifa. Alionya mapuuza kama haya anaashiria yataleta athari hatari dhidi ya umma wa Afrika kama hayajarekibishwa mapema. Alisema katika siku za nyuma Mataifa Wanachama yaliahidi kuchangisha dola bilioni 22 kunyanyua kilimo katika Afrika, na mataifa hayo yanaonekana kushindwa kuzitekeleza ahadi hizo ambapo ni bilioni chache tu za mchango ulioahidiwa ulifanikiwa kufadhiliwa katika kipindi cha sasa. Mkurugenzi Mkuu wa UNCTAD amesisitiza mchango wa kimataifa kwa wakulima wa Afrika, ni lazima ukamilishwe mwaka huu, ili kusaidia kuwasilisha mapinduzi ya zaraa, kama ilivyofanyika katika nchi za bara la Asia, au si hivyo njaa itaendelea kutota na kuselelea kwa kima kitachozusha janga hatari kwa maisha ya umma wa Afrika.