Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walimwengu waandamana kuunga mkono juhudi za WFP kupiga vita njaa duniani

Walimwengu waandamana kuunga mkono juhudi za WFP kupiga vita njaa duniani

Ijumapili ya tarehe 07 Juni (2009) makumi elfu ya watu, katika sehemu mbalimbali za dunia, walikusanyika kwenye miji kadha ya kimataifa, na kuandamana kuunga mkono juhudi za Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) katika kupiga vita tatizo la njaa ulimwenguni, hususan miongoni mwa watoto wadogo.

Kwa mujibu wa taarifa za UM, tukio hili la kila mwaka - liliopewa mada isemayo ‘Tutembee Dunia Nzima: Kukomesha Njaa' - lilikusanyisha jumla ya watu wanaokadiriwa 300,000 katika nchi 70, wanaoishi kwenye kanda zote 24 za majira ya saa tofauti, waliofanyisha maandamano karibu 200, matukio yaliofadhiliwa na washiriki wenzi kutoka makampuni ya binafsi ya TNT, Unilever na DSM. Maandamano makubwa hasa yalifanyika katika mataifa ya Afrika, ambapo watu 64,000 waliripotiwa kuandamana katika sehemu 53 mbalimbali nchini Malawi, na watu 50,000 waliandamana kwenye mji wa Arusha, Tanzania, wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizongo Kayanza Peter Pinda. Na katika Kenya, Balozi Mfadhili wa WFP dhidi ya Njaa, Paul Tergat - aliye bingwa wa mbio za masafa marefu za marathon, alijiunga pia na waandamanaji kadhaa katika mji wa Nairobi, kutetea haki ya kukomesha njaa.