Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu watatu wanyongwa hadharani Gaza

Watu watatu wanyongwa hadharani Gaza

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, (OHCHR), imelaani vikali kunyongwa kwa watu watatu na mamlaka ya Gaza jana Alhamisi, kwa hatia ya kuhusika na mauaji ya kiongozi wa Hamas, Mazen Al Faghaa mnamo Machi 24 pamoja na kushirikiana na chama adui.

Ofisi hiyo imesema adhabu hiyo iliyotolewa na "mahakama ya kijeshi" ni kinyume cha sheria ya kimataifa ya adhabu ya kifo, hukumu ambayo mahakama hiyo hairuhusu kukata rufaa wala kusamehewa, kitendo ambacho pia ni uvunjaji wa sheria za kimataifa.

kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu sheria ya kimataifa imeweka masharti magumu katika matumizi ya adhabu ya kifo, ikiwa ni pamoja na kufuata kwa kina viwango sawa katika kesi, lakini kesi hii haikuzingatia viwango hivyo, ikiongeza kuwa kipengele cha 109 cha sheria ya Palestina kinahitaji hukumu ya unyongaji iidhinishwe na rais, sheria ambayo pia imepuuzwa.

Ofisi hiyo imetoa wito kwa mamlaka ya Gaza kusitisha tabia ya mara kwa mara ya unyongaji wa watu, na pia matumizi ya mahakama ya jeshi na kuzingatia majukumu yake chini ya sheria ya kimataifa.