Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulinzi wa tabaka la Ozoni ni kwa manufaa yetu sote- Ban

Ulinzi wa tabaka la Ozoni ni kwa manufaa yetu sote- Ban

Dunia imebadilika tangu tuadhimishe kwa mara ya mwisho siku ya tabaka la Ozoni, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika ujumbe wake wa siku ay tabaka hilo hii leo.

Ban amesema mabadiliko hayo ni kama vile kupitishwa kwa ajenda 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu au SDGS, ambayo yatasaidia kuboresha hali ya maisha ya watu maskini ulimwenguni.

Ametaja pia mkataba wa mabadiliko ya tabianchi nchi au mkataba wa Paris ambao amesema umefungua ukurasa mpya katika safari ya dunia endelevu na yenye usalama.

Katibu Mkuu amesema kilichosalia sasa ni kuelekeza nguvu katika kusimamia mkataba wa Montreal wa kudhibiti gesi chafuzi kwa anga au HFCs.

Amesema nchini Rwanda mwezi ujao, wajumbe wa mataifa wana nafasi ya kukubaliana kwa ujumla na maafikiano ya mkataba wa Montreal na kupunguza hewa hizo akisema kuwa manufaa ya kupunguza HFCs sio tu kwa tabaka la Ozoni bali pia kutapunguza ongezeko la joto duniani.

Kwa mantiki hiyo amesema katika siku ya kulinda tabaka la Ozoni, kila mmoja akumbuke hatua bora za kuendelea kujenga dunia bora kwa kila mtu.