Twasubiri kwa hamu ziara ya Baraza la Usalama Sudan Kusini- Loej
Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS Bi Ellen Margaret Loej amesema ziara ya Baraza la Usalama itakayoanza nchini humo kesho Jumamosi, itawapa fursa ya kuona changamoto zinazowakabili watu wa Sudan Kusini hususan wale walio ndani ya kituo cha ulinzi wa raia.
Akihojiwa na Radio Miraya iliyo chini ya UNMISS, amesema anatarajia watakuwa na mazungumzo na vikundi vya kiraia ili kupata picha halisi kuhusu hali ya usalama, haki za binadamu na changamoto zingine zinazokumba raia.
Halikadhalika watapata fursa ya kusikia kutoka serikali ya mpito kuhusu wasiwasi ama changamoto zao katika kupata msaada kutoka UNMISS, utekelezaji wa mamlaka mpya za ujumbe huo pamoja na mkataba wa amani.
(Sauti ya Ellen)
"Baraza la usalama, kama ilivyo kwetu sisis hapa, limekuwa na wasiwasi mkubwa juu ya kuendelea kwa mapigano katika maeneo mbalimbali ya nchi. Tuna wasiwasi na hali ya usalama na ya kibinadamu , hivyo ni matumaini yetu kuwa ziara hii itatoa msukumo wa majadiliano ya wazi, juu ya namna bora serikali na Umoja wa Mataifa wanaweza kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya watu wa Sudan Kusini."
Bi. Loej amesema ziara hiyo ya siku tatu Sudan Kusini inakuja wakati muafaka ambapo wanakaribia kuwasilisha ripoti ya UNMISS kwa Katibu Mkuu.
Kutoka Sudan Kusini, wajumbe wa Baraza la Usalama wataelekea Addis Ababa, Ethiopia kwa mazungumzo tarehe Tano Septemba na Muungano wa Afrika kabla ya kurejea New York, Marekani.