Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MICT yaungana na dunia kukumbuka miaka 22 ya mauaji ya kimbari ya Rwanda

MICT yaungana na dunia kukumbuka miaka 22 ya mauaji ya kimbari ya Rwanda

Utaratibu wa mahakama za kimataifa za uhalifu (MICT) umeungana na dunia leo kukumbuka miaka 22 ya mauaji ya kimbari ya Rwanda yaliyotokea mwaka 1994 ambapo Watutsi na Wahutu na wengine waliopinga mauaji hayo waliuawa.

MICT imeshiriki misa maalumu ya kumbukumbu kwenye makao makuu ya jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) iliyoandaliwa na jumuiya ya watu wa Rwanda mjini Arusha Tanzania.

Hafla hiyo imeambatana na kuweka shada la maua na uwashaji wa mishumaa pia hotuba mbalimbali zilizozingatia kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni “pambana na mtazamo wa mauaji ya kimbari”

Miongoni mwa waliozungumza ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dr. Richard Sezibera, mwendesha mashitaka wa zamani wa mahakama ya kimataifa ya mauaji ya Kimbari ya Rwanda ICTR Hassan B. Jallow, na mkuu wa MICT tawi la Arusha bwana Samuel Akorimo, ambaye amesema ni lazima kuelimisha umma, kupambana na ukwepaji sheria na kuzuia migawanyiko ya kikabila na ghasia kuepuka kutokea tena kwa mauaji ya kimbari Rwanda na kote duniani.

MICT inaendelea na majukumu kadhaa ya ICTR baada ya mahakama hiyo kufungwa rasmi.