Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mnyumbuliko wa kijenetiki kusaidia mazao na mifugo kustahimili mazingira:FAO

Mnyumbuliko wa kijenetiki kusaidia mazao na mifugo kustahimili mazingira:FAO

Rasilimali za kijenetiki zinaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuinua kiwango cha lishe duniani wakati huu ambapo mabadiliko ya tabianchi yanazidi kushika kasi kuliko ilivyotarajiwa, hiyo ni kwa mujibu wa chapisho la shirika la chakula na kilimo duniani, FAO.

FAO inasema rasilimali hizo zinatokana na mimea na wanyama na zikifanyiwa mnyumbuliko wa kijenetiki zinaweza kuongeza tija na ubora wa mazao, mifugo, mazao ya baharini na hata misitu kwani zitastahimili mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ongezeko la joto duniani.

Mathalani chapisho hilo linasema iwapo kiwango cha joto kinaongezeka, wakulima watahitaji mazao ambayo yanaweza kustahimili kiwango kikubwa cha joto, halikadhalika mifugo.

Hata hivyo FAO inaonya kuwa mwelekeo huo wa mazao na mifugo kubadilishwa ili kustahimili mazingira unapaswa uendane na kubadilisha malengo ya mipango ya kilimo ya uzalishaji kwa kuchanganya aina tofauti za mazao.