Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IAEA yakutana na mawaziri kujadili mustakabali wa matumizi ya nyuklia

IAEA yakutana na mawaziri kujadili mustakabali wa matumizi ya nyuklia

Pakua

Shirika la kimataifa la nguvu za atomiki IAEA, limefungua  rasmi hii leo huko Abu Dhabi, Falme za kiarabu, mkutano wa kimataifa wa karne ya 21 wa nguvu za nyuklia unaojumuisha mashirika matano ya kimataifa,  mawaziri kutoka nchi 67  duniani na wajumbe kutoka asasi za kiraia wapatao 700, ili kujadili matumizi ya nguvu za  nyuklia  katika dunia ya sasa.

Mkurugenzi Mkuu wa  IAEA Yukiya Amano amesema nchi zilizoendela na zinazoendela lazima zijiwekee akiba ya kutosha ya nguvu za nyuklia ili kuendesha uchumi wa nchi zao hususani katika  uzalishaji wa umeme ambao ndio msingi wa uchumi wa kisasa.

Amesema hii ni moja wa makubaliano katika mkataba wa Paris katika kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa duniani.

Katika mkutano huu, mawaziri na viongozi waandamizi kutoka nchi wanachama wa IAEA watahusika katika majadiliano juu ya mkakati ya nishati ya nchi zao, nafasi ya nguvu za nyuklia,  changamoto zake  na operesheni za upanuzi.  Aidha, vikao  vigine kutoka asasi  mbalimbali vitajadili nguvu za nyuklia na maendeleo endelevu.

Mkutano huu ni wa nne kwa ngazi ya  mawaziri kufuatia mikutano ya awali huko Paris mwaka wa 2005, Beijing mwaka 2009 na St. Petersburg Urusi  mwaka 2013.

Halikadhalika mkutano huu unafanyika kwa  ushirikiano kati ya shirika la nishati ya nyuklia (NEA), na serikali ya Falme za Kiarabu kupitia wizara ya nishati na namlaka ya shirikisho kwa kanuni za Nyuklia.

Photo Credit
Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Yukiya Amano aakihutubia kikao cha ufunguzi wa Mkutano wa Waziri wa Kimataifa wa IAEA juu ya Nguvu ya Nyuklia katika karne ya 21 huko Abu Dhabi, UAE. (Picha: D. Calma / IAEA)