G5 ni rasilimali kwa waafrika- Balozi Delattre

20 Oktoba 2017

Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Oktoba Balozi François Delattre amesema kikosi cha pamoja dhidi ya ugaidi huko Sahel ni muhimu katika kupambana na ugaidi ambao hautambui mipaka.

Balozi Delattre amesema hayo akizungumza na wanahabari huko Bamako, Mali ambako wajumbe wa Baraza la Usalama wameanza ziara ya kutathmini pamoja na mambo mengine utekelezaji wa makubaliano ya amani na kuanza kwa kikosi hicho kinachoundwa na nchi 5 za ukanda huo au G5.

Nchi hizo ni Mali, Mauritania, Niger, Burkina Faso na Chad.

(Sauti ya Balozi Delattre)

“Mjumuiko wa jeshi hilo ni rasilimali kwa waafrika katika vita ambayo haitambui mipaka hapa Sahel. Kitisho cha ugaidi pia kinaathiri Ulaya na dunia nzima na hivyo ni wajibu ambao Ufaransa inaamini, ni wajibu wa jumuiya ya kimataifa na pia Baraza la Uaslam linasaidia jeshi hili ili liwe na uwezo unaotakiwa kukabili ugaidi ipasavyo.”

Halikadhalika wajumbe hao watakutana na pande kinzani ili kuwapatia ujumbe dhahiri wa umuhimu wa kuchagiza utekelezaji wa makubaliano ya amani na maridhiano yam waka 2015.

Kutoka Mali wataenda Mauritania na Burkina Faso ili kuangalia harakati za kuanza kazi kwa jeshi hilo la nchi tano au G5.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud