Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahojiano

Hadhi mpya ya Palestina ndani ya Baraza Kuu la UM kuchochea amani Mashariki ya Kati

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi tarehe 29 Novemba ambayo ni siku ya kimataifa ya kusimama bega kwa bega na Palestina, lilipitisha azimio la kuipatia Palestina hadhi ya uangalizi bila haki ya kupiga kura katika Baraza hilo.

Katika kura hiyo ya kupitisha azimio hilo, nchi 138 ziliunga mkono huku Tisa zikipinga na nchi 41 zikiwa hazikuonyesha msimamo wowote. Nchi zilizopiga kura ya hapana ni pamoja na Marekani na Israeli huku Uingereza na Hungary zikiwa miongoni mwa nchi ambazo hazikuonyesha msimamo wowote.

Madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa yaweza kuwa kichocheo cha kudhibiti utoaji gesi chafuzi

Mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa unafanyika Doha, Qatar suala kubwa likiwa ni hatua za kuchukua kupunguza gesi chafuzi zinazochochea ongezeko la joto duniani. Wakati hilo likijdaliwa, shirika la mpango wa Mazingira katika Umoja wa Mataifa, UNEP, limetoa taarifa inayozungumzia uwezekano wa kuyeyuka kwa kasi kubwa kwa udongo wenye barafu, Permafrost, ulioko kwenye maeneo ya kaskazini mwa dunia kitendo ambacho kitatoa hewa aina ya Methani yenye madhara zaidi kwa dunia kuliko hewa ya ukaa.

Kampeni ya 'Mimi pia ni mhamiaji', Afrika Kusini: IOM

Nchini Afrika kusini, Shirika la Uhamiaji la kimataifa, IOM kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR wanaanzisha kampeni iitwayo, Mimi pia ni mhamiaji yenye lengo la kuhamasisha raia wa nchi hiyo wafahamu kuwa wahamiaji nao pia ni sehemu ya jamii yao na hivyo kuleta utangamano miongoni mwa wakazi wote.

Kampeni hiyo itaendelea hadi tarehe 18 mwezi ujao ambayo ni siku ya kimataifa ya wahamiaji, ikijikita zaidi kuelimisha kuwa kimsingi raia wote wa Afrika Kusini ni wahamiaji au wana uhusiano na wahamiaji.