Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

UN Photo/Ariane Rummery

Kila uwekezaji uwe jawabu kwa changamoto za mabadiliko ya tabianchi- Ban

Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kumefanyika mkutano wa viongozi wa uwekezaji katika sekta binafsi lengo likiwa ni kuangalia hatari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya biashara.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema amesimama mbele ya wawekezaji hao akiwa na matumaini mapya kuwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma unaweza kukabili changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

UNMAS yalaani mashambulizi dhidi ya timu wategua mabomu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia huduma za kutegua mabomu ya kutegwa ardhini UNMAS limelaani vikali shambulio katika jimbo la Helmand nchini Afghanistan lililolenga timu ya kudhibiti mabomu ya kutegwa ardhini nchini humo DAFA.

Taarifa ya UNMAS imesema kuwa shambulio hilo pia lilielekezwa kwa asasi isiyo ya kiserikali ya udhibiti wa mabomu ya kutegwa ardhini pamoja na wadau wa mpango wa operesheni ya kung’oa mabomu ya kutegwa ardhini.

Mkutano wa sanyansi na teknolojia wa UNISDR umeanza leo Geneva

Mkutano wa sayansi na teknolojia wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya upunguzaji wa hatari ya majanga UNISDR umeanza leo mjini Geneva kwa kuwaenzi mamia ya wanasayansi ambao wamechangia muda wao kwa utafiti kuhusu mabadiliko ya tabianchi na athari zake.

Mkuu wa UNISDR bw. Robert Glasser, amesema kazi ya mamia ya wanasayansi waliochangia kwenye jopo la kimataifa la mabadiliko ya tabia nchi ni mfano bora dhahiri wa huduma kwa umma na kujitolea kwa mambo mema yanayotarajiwa kutoka kwa jumuiya ya kimataifa ya wanasayansi.

Mbinu za kisasa zahatarisha kutoweka kwa aina asilia za wanyama:FAO

Ripoti mpya ya shirika la chakula na kilimo duniani, FAO imesema kitendo cha wafugaji na watunga sera duniani kote kuvutiwa na mbinu za kisasa ili kuwa na aina bora ya wanyama katika zama za sasa za ongezeko la joto duniani kunatishia uwepo wa mbegu asilia za wanyama.

FAO imesema jamii zinatumia mbinu kama vile kuchanganya mbegu za wanyama ili kupata mbegu bora na kuhakikisha upatikanaji wa chakula lakini kuna matukio ambapo wataalamu na wafugaji wanapendezewa na aina moja zaidi.

Kumbukizi ya Holocaust, Ban atoa ujumbe jamii iache kubagua

Ikiwa leo  ni siku ya kimataifa ya kumbukizi ya wahanga na manusura wa mauaji ya halaiki ya Holocaust, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kumbukizi hii inadhihirisha kile kinachoweza kutokea iwapo binadamu atasahau utu wao.

Katika ujumbe wake Ban amesema mauaji ya Holocaust dhidi ya wayahudi yalikuwa uhalifu mkubwa ambao hadi sasa hakuna mtu anayeweza kupinga kuwa yalitokea na hivyo kumbukizi yake ni hatua ya kurejelea azma ya kuzuia vitendo hivyo visitokee tena.

Wajumbe wa Baraza la Usalama wafika Gitega kukutana na Rais

Wakiwa ziarani Afrika, wajumbe wa Baraza la Usalama wametembelea Burundi ambako wamejadili na wawaklishi wa vyama vya upinzani, asasi za kijamii, na rais wa Burundi Pierre Nkurunziza mustakhbali wa nchi hiyo ambayo sasa iko mzozoni.

Mkutano wa faragha na Rais Nkurunziza ulifanyika nje ya mji mkuu Bujumbura kwenye eneo tulivu la Gitega.

Safari hiyo ya Gitega na maoni ya wanachama wa Baraza la Usalama vinaripotiwa na Priscilla Lecomte kwenye makala hii.

Vitendo vya ukiukaji wa haki vyaongezeka DRC

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, imeorodhesha visa 347 vya ukiukaji wa haki za binadamu mwezi Disemba mwaka 2015 nchini humo.

Kwa ujumla, idadi ya visa hivyo imefika 3,877 mwaka uliopita, ikiwa ni ongezeko la asilimia 64 ikilinganishwa na mwaka 2014.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo, nusu ya vitendo hivyo vimetekelezwa na vikosi vya usalama vya serikali, huku zaidi ya askari 300 wa serikali wakiwa wameshtakiwa kwa vitendo hivyo mwaka 2015.

Wahamiaji wa Somalia na Ethiopia watumikishwa Yemen

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR nchini Yemen, Johannes van der Klaauw, ameeleza kwamba baadhi ya watu waliokimbilia Yemen kutoka Somalia na Ethiopia wanaripotiwa kutumikishwa vitani na waasi nchini humo.

Bwana Van der Klaauw amesema hayo akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa, huku akiongeza kwamba wengi wa wahamiaji hawana habari ya vita vinavyoendelea nchini humo kabla ya kufikia kwenye boti zinazowavukisha kwenda Yemen. Hata hivyo amesema wengi wao wanajaribu kuvuka Yemen na kufika Saudia, lakini safari hiyo ni hatari mno.

UM na mashirika ya misaada waomba dola milioni 298 kwa ajili ya wakimbizi Iraq:

Kukiwa hakuna mwangaza wa kuitisha vita nchini Syria Umoja wa Mataifa na mashirika ya kibinadamu na mae ndeleo nchini Iraq wametoa ombi la dola milioni 298 kwa ajili ya kuendelea na msaada kwa takribani wakimbizi 250,000 wa Syria walioko nchini Iraq.

Ombi hilo limetolewa katika uzinduzi wa mpango wa ukurasa mpya wa Iraq katika kusaidia wakimbizi wa Syria kikanda ujulikanao kama 3RP uliofanyika mjini Erbili. Watu mbalimbali wamehudhuria uzinduzi huo akiwemo Dr. Ali Sindi, waziri wa mipango wa serikali ya kikanda ya Kurdistan.

Hofu ya kirusi Zika, WHO yaitisha mkutano.

Shirika la Afya Duniani, WHO tarehe 28 mwezi huu litaitisha mkutano maalum kuhusu kirusi aina ya Zika. Amesema leo msemaji wa WHO Christian Lindmeier, wakati huu ambapo kirusi hicho tayari kimeripotiwa kwenye nchi 20 huku Brazil ikiwa ni nchi iliyoathirika zaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Geneva, Bwana Lindmeier ameeleza kwamba kirusi chenyewe cha Zika si hatari, kwani huhasababisha tu ukurutu mwilini.