Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: MONUSCO yafunga rasmi virago Kivu Kusini, yasalia Ituri na Kivu Kaskazini

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini DRC, Bintou Keita (kulia) akikabidhi kwa  Gaston Cisse wa Numbe kutoka ofisi ya Gavana wa Jimbo la Kivu Kusini hati ya kituo cha ulinzi cha Kavumu kilichokuwa kinatumiwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa k…
MONUSCO/Jean-Claude Wenga
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini DRC, Bintou Keita (kulia) akikabidhi kwa Gaston Cisse wa Numbe kutoka ofisi ya Gavana wa Jimbo la Kivu Kusini hati ya kituo cha ulinzi cha Kavumu kilichokuwa kinatumiwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Pakistani. Hii ilikuwa tarehe 25 Aprili 2024.

DRC: MONUSCO yafunga rasmi virago Kivu Kusini, yasalia Ituri na Kivu Kaskazini

Amani na Usalama

Operesheni za kijeshi za ulinzi wa amani zilizokuwa zinafanywa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC huko jimboni Kivu Kusini zimekamilika Jumanne ya Aprili 30, 2024 kwa mujibu wa azimio namba 2717 la mwezi Desemba 2023, la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Taarifa ya MONUSCO iliyotolewa Kinshasa, mji mkuu wa DRC, inasema azimio la Baraza la Usalama lilizingatia ombi la serikali ya taifa hilo la Maziwa Makuu.

Vikosi vya ulinzi wa amani vya MONUSCO vilianza kuondoka taratibu Kivu Kusini kuanzia mwezi Januari mwaka huu na hivyo kuanzia leo tarehe Mosi mwezi Mei jukumu la ulinzi wa raia linakoma kwenye jimbo hilo.

Wanaosalia ni watumishi waliovalia sare za usalama ambao watawajibika kuhakikisha ulinzi wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, mitambo na misafara ya Umoja wa Mataifa hadi pale MONUSCO itakapoondoka kabisa DRC mwezi Desemba mwaka huu.

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Bintou Keita ametangaza kuwa kuanzia sasa huko jimboni Kivu Kusini wajibu wa ulinzi na usalama wa raia unabakia kwa jeshi la ulinzi na usalama la DRC ambalo litaendelea kushirikiana na jamii na mamlaka za eneo hilo.

Wakati MONUSCO inaondoka, vikosi vya ulinzi na usalama vya serikali vinaimarisha na kuongeza uwepo wao kwenye maeneo ambayo MONUSCO inaondoka.

Sasa MONUSCO imesalia na majukumu ya ulinzi wa amani na raia kwenye majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini.

Azimio la Baraza la Usalama linataka MONUSCO iwe imeshaondoka DRC ifikapo Desemba 20 mwaka huu wa 2024.