Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya usalama mashariki mwa DRC bado si shwari- UN

Helikopta ya MONUSCO yatua Beni katika eneo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
UN Photo/Michael Ali
Helikopta ya MONUSCO yatua Beni katika eneo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hali ya usalama mashariki mwa DRC bado si shwari- UN

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limejulishwa kuwa hali ya usalama huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC inazidi kuwa mbayá wakati huu ambapo vikundi vya waasi vinashamirisha mashambulizi dhidi ya raia katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa nchini DRC Bintou Keita amesema hayo akiwasilisha ripoti ya Katibu Mkuu huku akitaja baadhi ya vikundi hivyo kuwa ni M23, Zaïre, CODECO na ADF.

Mashambulizi yamefurusha watu 900,000 Kivu Kaskazini 

Amesema huko Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri mamia ya maelfu ya raia wamekimbia mashambulizi kutoka vikundi hivyo vilivyojihami na mapigano kati ya M23 na jeshi la serikali FARDC. 

Halikadhalika mapigano kati ya CODECO na kikundi Zaïre. 

“Hasa katika jimbo la Kivu Kaskazini, mapigano kati ya waasi wa M23 na FARDC yamelazimu watu 900,000 kukimbia makazi yao na mahitaji ya  kibinadamu ambayo tayari ni makubwa DRC, yanazidi kuongezeka,” amesema Bi. Keita. 

Lakini cha kusikitisha amesema mahitaji hayo ya kibinadamu ni moja ya mahitaji yaliyopuuzwa zaidi duniani kwani wakimbizi hao wanaishi kwenye mazingira dhalili. 

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini DR Congo, Bintou Keita, (kushoto) akiwa na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa ziara  yao nchini humo.
MONUSCO
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini DR Congo, Bintou Keita, (kushoto) akiwa na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa ziara yao nchini humo.

Bi. Keita ambaye pia ni Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC ametumia kikao hicho kuomba kufadhiliwa kwa ombi la mwaka huu la usaidizi wa kiutu nchini humo ambalo ni takribani dola milioni 2.25. 

Makundi kinzani yaache kushambulia UN 

Pamoja na changamoto na ukata amesema juhudi za Umoja wa Mataifa za kupeleka msaada hata ulioko zinakwamishwa akirejelea shambulio la ndege ya Umoja wa Mataifa ya kupeleka misaada ya kibinadamu, UNHAS ambayo ilishambuliwa mwezi Februari na kulazimu shirika la Umoja wa  Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP kusitisha kwa musa safari zake kwenye maeneo yenye mizozo. 

“Nalaani vikwazo vyote vinavyoendelea dhidi ya ufikishaji wa misaada ya kibinadamu,” amesema Mkuu huyo wa MONUSCO huku akitoa wito kwa pande zote zinazokinzana kwenye mzozo huo kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu. 

MONUSCO imejipanga upya 

Baraza pia limejulishwa kuhusu mkakati wa MONUSCO wa kuweka vikosi kwenye maeneo hatarishi ili kukabiliana na ongezeko la ukosefu wa  usalama kwenye eneo la Djugu jimboni Ituri. 

“Tumeweka vikosi vya mapigano huko Kambala na Bokuku kukabili ukosefu wa usalam eneo la Djugu na vile vile kurahisisha mienendo ya wakimbizi wa ndani, sambamba na njia za kupitisha misaada ya kibinadamu,” amesema Bi. Keita akitaja mikakati hiyo. 

Hata hivyo ametoa wito kwa serikali kuimarisha vikosi vyake ya kijeshi na polisi vinavyopelekwa  huko Ituri na isongeshe jitihada zake za kushughulikia vitisho dhidi ya raia kutoka vikundi vilivyojihami kwenye majimbo hayo. 

Vilipuzi vinavyotegwa 

MONUSCO pia ilichukua hatua haraka dhidi ya mashambulio ya kigaidi kutoka waasi wa ADF kwenye mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini ambako wanatumia vilipuko vya kutengeneza. 

Bi. Keita amesema MONUSCO ilitoa huduma ya kutegua mabomu na huduma ya kusafirisha raia kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Huko jimboni Kivu Kusini MONUSCO imejikita kabisa kulinda wakimbizi wa ndani huko Bijombo na Mikenge. 

Ufanisi wa MONUSCO unategemea ushirikiano 

Katika hotuba yake, Bi. Keita ameeleza kuwa mwaka 2022 ulikuwa mwaka mbaya zaidi MONUSCO kwenye rekodi ya walinda amani kwani wanafanya kwenye mazingira magumu, hatari na mara nyingi walinda amani wetu ndio wanalipa gharama. “Napenda kutoa shukrani zangu kwa walinda amani wetu wanaojitolea na vile vile kurejelea rambirambi zangu kufuatia kifo cha mlinda amani wa UN kutoka Afrika Kusini aliyeuawa kwenye shambulio dhidi ya helikopta ya MONUSCO karibu na Goma mwezi Februari mwaka huu.” 

Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu wa UN nchini DRC amesisitiza kuwa ufanisi wa MONUSCO unategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa karibu na uwazi kutoka jeshi la serikali FARDC na majeshi ya kigeni yaliko nchini humo, iwe kupitia uhusiano kati ya nchi n anchi au kupitia jeshi la kikanda la Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC ili kuhakikisha kuna uratibu bora wa mipango na usalama na usimamizi wa haki za binadamu. 

Baraza ungeni mkono juhudi za kikanda 

Lakini amekumbusha kuwa operesheni za kijeshi pekee hazitaleta amani ya kudumu DRC huku akiunga mkono juhudi za kikanda ambazo ameomba Baraza la Usalama liunge mkono. 

Ametumia kikao hicho pia kutakia kila la kheri serikali mpya iliyoundwa na Rais Félix Tshisekedi wa DRC katika kutekeleza program zake na kwamba MONUSCO inasalia na azma yake ya kusaidia serikali katika kuimarisha usalama na kupokonya silaha, kuvunja makundi na kujumuisha wapiganaji wa zamani kwenye jamii, DDR.