Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Walinda amani wa UN kutoka China waondoka Kivu Kusini

Bintou Keita, Special rep wa SG DRC akimvalisha medali mmoja wa walinda amani wa UN kutoka China walikamilisha jukumu lao leo huko jimboni Kivu Kusini mashariki mwa DRC.
MONUSCO
Bintou Keita, Special rep wa SG DRC akimvalisha medali mmoja wa walinda amani wa UN kutoka China walikamilisha jukumu lao leo huko jimboni Kivu Kusini mashariki mwa DRC.

DRC: Walinda amani wa UN kutoka China waondoka Kivu Kusini

Amani na Usalama

Baada ya huduma ya ulinzi wa amani kwa zaidi ya miaka 20 huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO, walinda amani kutoka China, hii leo wameondoka kutoka kambi yao iliyoko nje kidogo ya mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, Bukavu ambako walishiriki kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa miundombinu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani hii leo, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema hafla ilifanyika hii leo kwenye kituo chao kutoa shukrani kwa mchango wa walinda amani hao katika kuimarisha amani na usalama jimboni Kivu Kusini. 

Kuondoka kwao ni sehemu ya mpango wa MONUSCO kufunga virago DRC kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo ujumbe huo unatakiwa uwe umekamilisha majukumu yake mwezi Desemba mwaka huu ambapo kuondoka kumeanza mapema mwezi Januari mwaka huu. 

Mchango wa walinda amani wa UN kutoka China

Kwa mujibu wa redio Okapi, ambayo iko chini  ya MONUSCO, walinda amani hao wa Umoja wa Mataifa kutoka China, tangu mwaka 2003 wamesaidia kuimarisha miundombinu kadhaa ikiwemo kukamilisha zaidi ya miradi 580 ya uhandisi, kukarabati kilometa 1,800 za barabara, kukarabati zaidi ya madaraja 80 na ujenzi aw viwanja 20 vya helikopta.

Mchango wao ulifanikisha utekelezaji wa majukumu ya MONUSCO jimboni Kivu Kusini.

Mkuu wa MONUSCO, Bintou Keita ambaye pia ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini DRC, ameelezea shukrani zake za dhati kwa China kwa kupeleka walinda amani wake waliopelekewa Kivu Kusini ambao amesema wamejitofautisha wenyewe kwa ueledi wao kiteknolojia, kikazi na nidhamu katika kukabili changamoto walizokumbana nazo, na wakati mwingine walifanya kazi kwenye mazingira magumu.

"Wamechangia kwa dhati amani na usalama DRC,” amesema Bi. Keita.

Bi. Keita pia amesisitiza azma ya MONUSCO kushirikiana na mamlaka za DRC katika kutekeleza mpango wake wa kuondoka nchii humo, akieleza kuwa kuondoka huo kutakuwa kwa umakini, kutafuata kanuni, kutakuwa na uwajibikaji na endelevu.

“Kuondoka kwa MONUSCO jimboni Kivu Kusini,hakumaanishi kuondoka kwa Umoja wa Mataifa,” amesisitiza. Badala yake kuondoka huko kunawakilisha upangaji upya wa uwepo wa  UN nchini humo ili  kuendelea kusaidia wananchi na serikali ya DRC.

Amesema baada ya MONUSCO kuondoka, mashirika ya UN yataendelea kusaidia kwa mujibu wa mamlaka waliyopatiwa huku serikali ya DRC ikibeba jukumu la ulinzi na usalama wa raia.

Azimio kuhusu kuondoka kwa MONUSCO

Tarehe 20 mwezi Desemba mwaka jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuongeza muda wa MONUSCO hadi tarehe 20 Desemba mwaka huu wa 2024, muda ambao ndio mwisho wa kuweko kwa ujumbe huo uliokuweko nchini humo tangu mwaka 2000.

Azimio linatambua mpango wa kina wa awamu tatu uliowasilishwa kwa Baraza la Usalama na serikali ya DRC na Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa nyaraka namba S/PRST/2023/5, na inatambua mpango wa MONUSCO wa kuanza kuondoa vikosi vyake jimboni Kivu Kusini ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2023 na kitakuwa kimekamilika kuondoka eneo hilo mwishoni mwa Aprili 2024.