Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali bado si shwari Mashariki mwa DRC, MONUSCO yaimarisha doria

Doria ya pamoja kati ya jeshi la serikali ya DRC, FARDC na MONUSCO huko jimboni Kivu Kaskazini.
MONUSCO / Alain Wandimoyi
Doria ya pamoja kati ya jeshi la serikali ya DRC, FARDC na MONUSCO huko jimboni Kivu Kaskazini.

Hali bado si shwari Mashariki mwa DRC, MONUSCO yaimarisha doria

Amani na Usalama

Mapigano yameendelea kuripotiwa kati ya jeshi la serikali nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na waasi wa kundi la M23 mashariki mwa nchi hiyo ambapo hapo  jana mapigano yalishika kasi kwenye eneo la Sake jimboni Kivu Kaskazini.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari mjini New York, Marekani ya kwamba mapigano hayo yalisababisha wakazi wengi wa Sake kukimbilia mji mkuu wa Kivu kaskazini, Goma, ilhali wengine walikimbilia jimbo la Kivu Kusini.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCI ulituma kikundi cha doria kwenye eneo kati ya Sake na goma na huku ukiendelea na juhudi za kulinda raia.

“Ujumbe huo pia unaendelea kuratibiana na wadau wa usaidizi wa kiutu ili kutathmini hali ya mahitaji na hatimaye kupunguza machungu kwa raia,” amesema Bwana Dujarric.

Mlinda amani wa UN kutoka Afrika Kusini aliyeuawa aagwa

Katika hatua nyingine, MONUSCO imesema hii leo wamekuwa na tukio la kuaga mwili wa mlinda amani wa Umoja wa Mataifa aliyeuawa wakati helikopta ya ujumbe huo iliposhambuliwa ikiwa njiani tarehe 5 mwezi huu wa Februari.

Bwana Dujarric amesema mwili wa Sajini Vusi Mabena utasafirishwa kesho Jumamosi Kwenda nyumbani Afrika Kusini.

Ujumbe wa ngazi ya juu na mazungumzo Kinshasa

Wakati huo huo, ujumbe wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa umekuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa DRC Jean-Michel Sama Lukonde Kyenge kwenye mji mkuu, Kinshasa.

Kwa mujibu wa Bwana Dujarric, ujumbe huo unajumuisha Msaidizi wa Katibu Mkuu wa UN kuhusu Afrika, Kiongozi wa ofisi ya kusaidia Ujenzi wa Amani, Elizabeth Spehar, na Alexandre Zouev, kutoka ofisi ya Utawala wa Sheria katika Idara ya Ulinzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa, halikadhalika Naibu Mkuu wa UNDP na Mkuu wa ofisi ya kanda ya Afrika, Ahunna Eziakonwa.

Mjadala wao ulijikita kwenye vipaumbele kama vile upokonyaji silaha na uvunjaji makundi ya waasi nchini humo, miradi ya kukwamua na kuweka utulivu kwenye jamii pamoja na michakato ya Nairobi na Luanda ambayo yote inalenga kupunguza mvutano na kuleta amani mashariki mwa nchi hiyo.

Michakato ya Nairobi na Luanda

Mchakato wa Nairobi, unaongozwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo hivi karibuni katika mkutano wa wakuu wa nchi uliofanyika nchini Burundi, viongozi hao walitoa taarifa ya pamoja ya kurejelea wito wao wa kutaka sitisho la mapigano kutoka kwa wapiganaji mashariki mwa DRC.

Na kwa upande wake, mchakato wa Luanda unaongozwa na Rais wa Luanda João Lourenço ambaye huwaleta pamoja Rais wa Rwanda Paul Kagame na Rais Felix-Antoine Tchisekedi Tshilombo pamoja na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika MAshariki na msuluhishi wa mzozo huo kutoka EAC ambaye ni Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Walijadili pia usaidizi wa UN kwa taifa hilo kwenye uchaguzi wa Rais unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

M23 haijaondoka kwenye maeneo kama ilivyoelezwa kwenye makubaliano

Waasi wa M23 wametwaa maeneo mengi katika jimbo la Kivu Kaskazini tangu mwezi Oktoba mwaka jana na kutishia kusonga hadi mji mkuu jimbo hilo, Goma.

Zaidi ya watu 500,000 wameripotiwa kufurushwa na kuwa wakimbizi wa ndani kwenye jimbo hilo tangu mwezi Machi mwaka jana na mapema wiki iliyopita, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis alifanya ziara yake ya kwanza nchini humo na kutoa wito kwa kukoma kwa ghasia.

Makubaliano yaliyotiwa saini mwezi Novemba mwaka jana pindi waasi hao walipokubali kujiondoa maeneo waliyotwaa bado hayajaza matunda.