Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muda wa MONUSCO waongezwa hadi Desemba 20, 2024; Majukumu yaainishwa

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa, Kikosi cha 9 kutoka Tanzania, TANZBATT 9 katika doria ya barabara ya Mbau-Kamango
TANZBATT 9
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa, Kikosi cha 9 kutoka Tanzania, TANZBATT 9 katika doria ya barabara ya Mbau-Kamango

Muda wa MONUSCO waongezwa hadi Desemba 20, 2024; Majukumu yaainishwa

Amani na Usalama
  • MONUSCO itakuweko hadi Desemba 20, 2024
  • Itaanza kuondoka mwishoni mwa mwaka huu huko Kivu Kusini
  • MONUSCO isaidie kwenye ufuatiliaji wa uchaguzi mkuu

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo kwa kauli moja limepitisha azimio namba 2717/2023 la kuongeza hadi tarehe 20 mwezi Desemba mwakani muda wa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC), MONUSCO, ujumbe ambao muda wake awali ulikuwa unamalizika leo. Rasimu ya azimio hilo iliwasilishwa na Ufaransa.

Azimio hilo lenye kurasa 16 linaweka bayana kuwa muda unaongezwa wa majukumu ikiwemo bila ya kukiuka  kanuni za msingi za ulinzi wa amani na Kikosi chake cha kujibu mashambulizi.

Kauli ya Mwakilishi wa kudumu wa DRC Umoja wa Mataifa

Akizungumza baada ya kupitishwa kwa azimio, Mwakilishi wa Kudumu wa DRC kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Zénon Mukongo Ngay, amesema, “tunashukuru sana Baraza la Usalama kwanza kabisa kwa kupokea ombi letu na kuchukua hatua kwa haraka. Ombi letu la kupanua wigo wa usaidizi wa vifaa kutoka MONUSCO hasa kwenye majimbo ambako awali ujumbe huo haukuweko chini ya majukumu yake, na kufanya hivyo wakati huu kunafanya mchakato wa uchaguzi uwe wa ufanisi.”

Amesema mchakato huo wa uchaguzi uliokuwa unaendelea na kufikia tamati kwa kampeni leo,  na sasa uchaguzi ndio unaanza kwa kuruhusu wananchi wa DRC kupiga kura kesho Desemba 20, 2023.

Kupungua kwa wanajeshi na watendaji

Aidha Baraza limeamua kuwa hadi tarehe 30 mwezi Juni mwaka 2024, kiwango cha juu cha idadi ya wanajeshi kitakuwa 13,500, waangalizi wa kijeshi na maafisa 660 na maafisa polisi 591 na askari polisi 1,410.

Hata hivyo kuanzia tarehe Mosi Julai 2024, idadi ya wanajeshi itapungua hadi 11,500, waangalizi wa kijeshi na maafisa 600, maafisa wa polisi 443, na polisi 1,270.

Majukumu ya kimkakati ya MONUSCO

Vipaumbele vya kimkakati vya MONUSCO ni viwili ambapo mosi; ni ulinzi wa raia kwenye maeneo ambako bado ipo ambayo ni majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri.

Pili; Kusaidia utulivu na kuimarisha taasisi za serikali nchini DRC ikiwemo marekebisho muhimu ya utawala na ulinzi.

Walnda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO wako chonjo kuhakikisha kuna usalama na hapa ni Djugu jimboni Ituru ambako walifika kuweka doria baada ya ripoti za kuweko kwa kikundi cha CODECO ambacho hushambulia raia.
MONUSCO/Force
Walnda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO wako chonjo kuhakikisha kuna usalama na hapa ni Djugu jimboni Ituru ambako walifika kuweka doria baada ya ripoti za kuweko kwa kikundi cha CODECO ambacho hushambulia raia.

Haki za binadamu na uchaguzi

Kwenye masuala ya haki za binadamu, azimio hilo pamoja na mambo mengine limemulika uchaguzi mkuu ambao unafanyika kesho DRC.

Azimio linaidhinisha MONUSCO kufuatilia, kutoa ripoti haraka kwa Baraza la Usalama na kufuatilia ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji hasa kwenye fursa za kisiasa na ghasia ikiwemo uchaguzi.

Mvutano kati ya DRC na Rwanda

Wajumbe pia kupitia azimio hilo wameelezea wasiwasi wao kuhusu kushamiri kwa ghasia mashariki mwa DRC na kuendelea kwa mvutano kati ya Rwanda na nchi hiyo huku likitambua kuwa DRC imeendelea kuathiriwa vibaya na mzunguko wa mashambulizi na ghasia kutoka vikundi vya kigeni na vya ndani vilivyojihami ikiwemo M23, CODECO na ADF.

Hivyo “Azimio linatoa wito wa utulivu na mazungumzo zaidi kati ya DRC na Rwanda ili kusongesha amani ya kudumu kwenye ukanda huo, na kusisitiza umuhimu wa uratibu na kusaidiana kwa mikakati ya kisiasa na usalama nchini DRC ikiwemo kwa usaidizi na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa UN Ukanda wa Maziwa Makuu na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini DRC.”

Walinda amani wa UN kutoka Bangladesh waokoa wachungaji wawili waliotekwa na wanamgambo pamoja na ng'ombe wao 23 katika kijiji cha Su, eneo la Djugu jimboni Ituri nchini DRC.
MONUSCO/Force
Walinda amani wa UN kutoka Bangladesh waokoa wachungaji wawili waliotekwa na wanamgambo pamoja na ng'ombe wao 23 katika kijiji cha Su, eneo la Djugu jimboni Ituri nchini DRC.

Kuondoka kwa MONUSCO

Azimio linatambua mpango wa kina wa awamu tatu uliowasilishwa kwa Baraza la Usalama na serikali ya DRC na Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa nyaraka namba S/PRST/2023/5, na inatambua mpango wa MONUSCO wa kuanza kuondoa vikosi vyake jimboni Kivu Kusini ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2023 na kitakuwa kimekamilika kuondoka eneo hilo mwishoni mwa Aprili 2024.

Halikadhalika limeamua kuanza kuondoka taratibu na kwa mpango kutoka DRC na kutekeleza mpango wa kukabidhi taratibu wajibu wake kwa serikali ya DRC.

Uwepo wa MONUSCO huko Kivu Kaskazini na Ituri utaanza kupungua kuanzia mwezi Mei mwaka 2024 na kuhitimishwa mwishoni mwa muda wa uwepo wa MONUSCO DRC Desemba 20, 2024.

Baraza limeiomba serikali ya DRC na Umoja wa Mataifa kupitia Kikosi kazi cha PAmoja kinachojumuisha serikali, MONUSCO na ofisi ya UN, DRC kuwa wamewasilisha taarifa tarehe 30 mwezi Juni 2024 kuhusu utekelezaji wa mpango wa kuondoka DRC na mapendekezo ya hatua za kufuata ili kuondoka huko kusisababishe changamoto.

Azimio limemtaka Katibu Mkuu wa UN awe anatoa ripoti kila baada ya miezi mitatu kuhusu utekelezaji wa azimio hili.