Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wa UN kutoka Pakistani waondoka DRC

Kikosi cha wanawake cha walinda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO kutoka Pakistani kikiwa kwenye doria huko Uvira, na Sange jimboni Kivu Kusini nchini DRC.
MONUSCO/Kevin Jordan

Amani na Usalama

Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kuondoa vikosi vya ulinzi wa amani vya umoja huo vinavyohudumu chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, (MONUSCO) linaendelea kutekelezwa ambapo hivi karibuni zaidi, wanajeshi walioondoka ni wale wa Pakistani.

Taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti wa MONUSCO, inasema takribani wanajeshi 277 kutoka Pakistani waliondoka Kivu Kusini wiki hii kurejea nyumbani kwao barani Asia.

Msemaji wa MONUSCO, Luteni Kanali Kedagni Menhsah, ametoa taarifa hizo akizungumza na waandishi wa habari mjini Goma, jimboni Kivu Kaskazini siku ya Alhamisi Machi 28.

Hii ni sehemu ya awamu ya kwanza 

Amesema kuondoka kwao ni sehemu ya awamu ya kwanza ya MONUSCO kujiondoa taratibu kwenye taifa hilo la Maziwa Makuu barani Afrika kufuatia ombi la serikali lililoungwa mkono na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

"Awamu zingine zitafuatia, bila shaka, vikosi vya ulinzi wa taifa vitajitahidi kwa kadri ya uwezo wake, hasa baada ya usaidizi ambao vimepatiwa kutoka ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa,” amesema Luteni Kanali Kedagni Menhsah.

Amesema MONUSCO kwa upande wake imejizatiti kutekeleza mamlaka mpya iliyopatiwa kuhusu awamu za kuondoka DRC, huku ikiruhusu jeshi la kitaifa la ulinzi na usalama kurejea kwenye majukumu yake kwa kujitegemea.

Kikosi cha wanawake cha walinda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO kutoka Pakistani kikiwa Uvira, na Sange jimboni Kivu Kusini nchini DRC  kuwapatia wanawake stadi za ushoni wa nguo.

Kamanyola na Lubero vimeshafungwa

Kituo cha MONUSCO cha Kamanyola, huko Kivu Kusini ambacho kilikuwa kinatumiwa na walinda amani hao wa Umoja wa Mataifa kutoka Pakistani kilifungwa tarehe 28 mwezi Februari mwaka huu na majengo yake kukabidhiwa ka Polisi wa kitaifa nchini humo, CNP.

Mwezi Desemba mwaka jana, MONUSCO pia ilifunga kituo chake kilichoko Lubero jimboni Kivu Kaskazini baada ya kuweko huko kwa miaka 21, kituo ambacho kilikuwa na vikosi vya walinda amani kutoka India, Afrika Kusini, Morocco na Nepal.

Azimio la kuondoka kwa MONUSCO nchini DRC

Tarehe 20 mwezi Desemba mwaka jana Baraza la Usalama la Umoja wa Matafa lilipitisha azimio la kuongeza muda wa MONUSCO hadi tarehe 20 Desemba mwaka huu wa 2024, muda ambao ndio mwisho wa kuweko kwa ujumbe huo uliokuweko nchini humo tangu mwaka 2000.

Azimio linatambua mpango wa kina wa awamu tatu uliowasilishwa kwa Baraza la Usalama na serikali ya DRC na Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa nyaraka namba S/PRST/2023/5, na inatambua mpango wa MONUSCO wa kuanza kuondoa vikosi vyake jimboni Kivu Kusini ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2023 na kitakuwa kimekamilika kuondoka eneo hilo mwishoni mwa Aprili 2024.

Bendera ya Umoja wa Mataifa ikikabidhiwa kwa maafisa wa MONUSCO nchini DRC kuashiria kufungwa kwa ofisi ndogo za ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda amani kwenye eneo hilo lililoko kilometa takribani 140 kutoka mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini.
UN/George Musubao

Uwepo wa MONUSCO huko Kivu Kaskazini na Ituri utaanza kupungua kuanzia mwezi Mei mwaka 2024 na kuhitimishwa mwishoni mwa muda wa uwepo wa MONUSCO DRC Desemba 20, 2024.

Baraza liliomba serikali ya DRC na Umoja wa Mataifa kupitia Kikosi kazi cha Pamoja kinachojumuisha serikali, MONUSCO na ofisi ya UN, DRC kuwa wawe wamewasilisha taarifa tarehe 30 mwezi Juni 2024 kuhusu utekelezaji wa mpango wa kuondoka DRC na mapendekezo ya hatua za kufuata ili kuondoka huko kusisababishe changamoto.

Azimio limemtaka Katibu Mkuu wa UN awe anatoa ripoti kila baada ya miezi mitatu kuhusu utekelezaji wa azimio hili.