Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO: Zaidi ya dola mil 16 kuwekezwa kwenye misitu nchini Uganda

Mwanamke anayejishughulisha na kilimo na ufugaji akimwagilia mazao nchini Uganda
© FAO/Luis Tato
Mwanamke anayejishughulisha na kilimo na ufugaji akimwagilia mazao nchini Uganda

FAO: Zaidi ya dola mil 16 kuwekezwa kwenye misitu nchini Uganda

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO limezindua mradi wa thamani ya euro milioni 15 sawa na dola milioni 16.29 unaofadhiliwa na Muungano wa Ulaya EU ili kusaidia sekta ya misitu ya Uganda kuchangia kwa uendelevu zaidi kwa uchumi na mazingira. 

Mpango wa miaka mitano wa Minyororo ya Thamani Endelevu ya malighafi za miti nchini Uganda, unalenga kuhakikisha upatikanaji endelevu wa malighafi halali za miti kutoka katika misitu iliyopandwa, kuongeza uwezo wa usindikaji na mahitaji ya soko ya bidhaa za mbao na kuboresha uwepo na upatikanaji wa ufadhili nafuu.

Balozi wa EU nchini Uganda Jan Sadek amesema muungano huo unajivunia dhamira yake ya kuendeleza uwekezaji katika sekta ya misitu kibiashara nchini humo. 

“Kwa kutumia juhudi za ushirikiano za Ushirikiano wa Misitu wa Timu yetu ya Ulaya na kutoa fedha za ziada kwa ajili ya usindikaji na uuzaji wa bidhaa za mbao, EU imejitolea kukuza ukuaji wa sekta imara na endelevu ambayo inastawi kimazingira na kibiashara,” alisema Balozi Sadek.

Ufadhili huu unakuja wakati ambao Uganda inakabiliwa na jinamizi la uvamizi, ukataji miti haramu na uharibifu wa misitu. 

Kwa mujibu wa FAO takriban robo moja ya ardhi ya Uganda ilikuwa msitu mwaka 1990 lakini hadi kufikia mwaka 2017 ilikuwa karibu nusu hadi kufikia asilimia 13 pekee na kwamba mradi huu utakuza upandaji miti na kuongeza thamani huku ukijenga utamaduni bora wa upandaji miti.

“Juhudi hizi zinalenga kuibua uwezekano wa rasilimali za misitu za Uganda kuchangia kwa uendelevu zaidi katika ukuaji wa uchumi shirikishi, juhudi za kimataifa za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na upotevu wa viumbe hai na kukuza uwezeshaji wa wanawake kiuchumi,” alisema Mwakilishi wa FAO nchini Uganda Antonio Querido.

FAO wamesema lengo lingine la mradi huo ni kufikia uchumi wa kiwango kwa kujumlisha zaidi wakulima wadogo wa miti nchini humo na wasindikaji wa kuni.

Soma zaidi kuhusu mradi huo hapa.