Tusipolinda bayoanuai dunia nzima itakuwa mashakani:UN

22 Mei 2019

Bayoanuai ni muhimu sana kwa afya ya binadamu na mustakbali wa dunia amesema leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake kwa ajili ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya bayoanuai akisisitiza kuwa sisitiza kuwa na viumbe vingine vyote katika mfumo wa maisha.

Ameongeza kuwa kuanzia maji tunayokunywa, chakula tunachovuta na hewa tunayovuta vyote vinategemea maliasili ya dunia iliyo katika afya njema. “ Tunahitaji mfumo wa maisha wenye afya kuweza kufikia malengo ya maendeleo endelevu SDGs na kushughulikia mabadiliko ya tabianchi  na inaweza kuchangia asilimia 37 ya jitihada zinazohitajika katika kudhibiti ongezeko la joto duniani.”

Hata hivyo amesema mfumo mzima wa maisha wa dunia hivi sasa unakabiliwa na changamoto na tishio kubwa ,na  ripoti mpya kutoka jukwaa la kimataifa la sayansi  na será kuhusu bayoanuai na huduma za mfumo wa maisha imeonyesha kwamba malia asili inapotea kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika historia ya binadamu.

Tangu mwaka 1990ukataji miti umesababisha kupotea kwa zaidi ya ekari milioni 290 za misitu ambazo zinasaidia kunyonya hewa ukaa kutoka hewani.  Ameongeza kuwa mimea milioni 1 na aina mbalimbali za wanayama viko hatarini kutoweka na asilimia zaidi ya 90 ya akiba ya samaki baharini inaanza kupungua au kuvuliwa kupita kiasi.

Athari za kutoweka kwa bayoanuai

Katibu Mkuu amesema athari zake kwa binadamu kote duniani ni mbaya sana. Mwenendo wa sasa mbaya wa bayoanuai na mfumo wa maisha vitakadiriwa kuathiri takribani asilimia 80 ya mchakato wa utimizaji wa malengo ya maendeleo endelevu au SDGs.”Na hatuwezi kuruhusu hili kutokea” amesisitiza Guterres.

Mwaka huu siku ya kimataifa ya bayoanuai “inaainisha athari za kutelekeza mazirira kwa uhakika wa chakula na afya ya jamii. Mfumo wa sasa wa chakula duniani umeathirika, mabilioni ya watu hawana fursa ya kupata lishe bora na takribani theluthi moja ya chakula kinachozalishwa kinapotea au kutupwa. Njia ambazo tumatumia kulima, kuandaa, kusafirisha, kutumia na kutupa chakula ndio sababu kubwa za kupotea kwa bayoanuai huku pia zikichangia katika mabadiliko ya tabianchi.”

Amesisitiza kwamba “Ni lazima tuchukue hatua haraka kubadili mwenendo huu na kuchagiza mwenendo unaofaa. Suluhu zipo, kwa kusitisha tabia zinazoathiri mazingira , kupanua wigo wa mchanganyiko wa kilimo chetu  na kuchagiza zaidi uzalishaji endelevu na mundo wa utumiaji, tunaweza kuimarisha afya ya kimataifa, kuongeza uhakika wa chakula na kuimarisha mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.”

Katibu mkuu ametoa wito akizitaka serikali zote duniani , makampuni ya biashara na asasi za kiraia kuchukua hatua haraka kulinda na kudhibiti hali tete na mfumo nyeti wa maisha kwenye dunia pekee tuliyonayo.

Umuhimu wa kulinda bayoanuai

Naye Katibu Mkuu wa mkuu wa shirika la kimataifa la mkataba wa bayoanuai Dkt. Cristiana Pasca Palmer akisisitiza umuhimu wa bayoanuai katika maisha ya kila siku , dunia na viumbe vyake amesema Siku hii inahimiza kazi ambayo sote tunapaswa kuifanya kila siku  na kila mwaka katika kuifufua, kuilinda na kuitumia vyema maliasili ya dunia ambayo inatupatia fursa muimu ya kuiita nyumbani kwani bayoanuai ni sehemu yetu kwani binadamu pia ni miongoni mwa maliasili.”

Ameongeza kuwa hivyo si kwa bahati mbaya kwamba kaulimbiu ya mwaka huu ya siku ya bayoanuai ikuwa “Chakula chetu, afya yetu na bayoanuai yetu” mada inayoonyesha uhusiano baina ya chakula binadamu wanaotumia, amustakabali wa afya zao na mazingira tunayoishi.

Kwa mantiki hiyo Dkt. Palmer amesema “tusipokuwa na bayoanuai bora hatuwezi kuwa na lishe bora , na bila lishe bora hatuwezi kuwa afya na maisha bora”

Ametoa wito kwa kila serikali, mashshirika, asasi za kiraia na watu binafsi kuchukua hatua stahiki kulinda bayoanuai kwani si tu kwamba itanusuru kizazi hiki bali pia kuokoa vizazi vijavyo.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud