Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Baraza la Mazingira Duniani UNEA6 wangoa nanga Nairobi Kenya

Mkutano wa Sita wa Wazi wa Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu (OECPR-6) huko Nairobi, Kenya.
UNEP / Eugene Kaiga
Mkutano wa Sita wa Wazi wa Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu (OECPR-6) huko Nairobi, Kenya.

Mkutano wa Baraza la Mazingira Duniani UNEA6 wangoa nanga Nairobi Kenya

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa sita wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEA6 leo umefungua pazia katika Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizopo jijini Nairobi, nchini Kenya.  Mkutano huo utakaodumu kwa siku tano unahudhuriwa na washiriki zaidi ya 6000 ikiwa ni pamoja na viongozi wa Mazingira duniani, asasi za kiraia, wataalamu wa Mazingira, maofisa waserikali za mitaa, wakulima, vyama vinavyowakilisha wafanyakazi, jamii zilizoachwa nyuma pamoja na maofisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa.

Irene Mwoga mtaalamu wa takwimu wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP kwa bara la Afrika ni Mratibu wa Mkutano huo amezungumza na Stella Vuzo wa kitengo cha habari cha Umoja wa Mataifa Naironi Kenya UNIS na kumweleza kuhusu dhamira ya mkutano huu unaofanyika kila baada ya miaka miwili, katika mwezi wa Februari .

Irene Mwoga mtaalamu wa takwimu wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP kwa bara la Afrika.
UNIS/Stella Vuzo
Irene Mwoga mtaalamu wa takwimu wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP kwa bara la Afrika.

Maduhui ya UNEA6 mwaka huu

Bi. Mwoga amesema “Kaulimbiu ya UNEA6 ni ushirikishwaji madhubuti na endelevu wa pande zote. Hii inamaanisha serikali, nchi washiriki, taasisi binafsi na makundi mbalimbali yakiwemo ya kina mama, taasisi za fedha na asasi za kiraia.”

Pia amesema kuhudu dhamira ya UNEA6 ni “kuweza kusikia sauti kutoka pande mbalimbali katika kutimiza malengo maalum za kukabiliana na changamoto za mazingira.”

Ameongeza kuwa katika mkutano huo kuna rasimu mbalimbali zimewasilishwa kwa ajili ya kujadiliana na pindi rasimu hizo zitakapokubaliwa pamoja na nchi washiriki na taasisi mbalimbali utekelezaji wake sasa ndio utakaoleta chachu na mbadiliko katika kuratibu sera, kupanga mikakati na kufuatilia jinsi mazingira yanavyoweza kulindwa kwa pamoja.

Amesema rasimu hizo zimegawanyika katika makundi makuu manne ambayo ni “Mosi ulindwaji wa rasilimali nchi kavu pamoja na baharini, pili kudhibiti matumizi ya plastiki na kemikali, tatu kuboresha ushirikiano wa kikanda ikiwa ushirikiano wa mabaraza ya mawaziri pamoja na ushirikiano na taasisi nyingine ambazo zinashirikiana na serikali katika kuboresha na kufanya miradi mbalimbali katika nchi washiriki.”

Mkutano wa sita wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEA6 jijini Nairobi nchini Kenya.
UNIS/Stella Vuzo
Mkutano wa sita wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEA6 jijini Nairobi nchini Kenya.

Ujumbe muhimu katika UNEA6

Mratibu huyo wa UNEA6 amesema kuna jumbe mbalimbali ambazo zimetolewa leo katika siku ya ufunguzi na kubwa zaidi ni kwamba “Mada kuu ya mazingira si mada ambayo inapaswa kushughulikiwa na chombo kimoja . Kwa hiyo tumeona kwamba kuna pande mbalimbali ambazo zinaweza zikachangia.”

Ameongeza kuwa pande hizo ni pamoja na sekta ya afya, maji na fedha. 

Na yote hiyo amesema ni katika kushirikisha nguvu na sauti za watu wa makundi mbalimbali kwa lengo la kutimiza dhambira ya kupambana na changamoto za mazingira.