Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo mapya kuhusu uchafuzi wa plastiki yanafanyika Nairobi: UNEP

Dandora huko Nairobi, Kenya, ambapo taka nyingi ni za plastiki. (Maktaba)
© UNEP
Dandora huko Nairobi, Kenya, ambapo taka nyingi ni za plastiki. (Maktaba)

Mazungumzo mapya kuhusu uchafuzi wa plastiki yanafanyika Nairobi: UNEP

Tabianchi na mazingira

Wanaharakati kutoka kote ulimwenguni wamekusanyika Nairobi, Kenya, kuanzia Jumatatu wiki hii kwa mazungumzo mapya juu ya mkataba wa kihistoria wa kimataifa wa kukabiliana na uchafuzi wa taka za plastiki.

Uharaka wa juhudi hizi unasisitizwa na mgogoro unaoendelea wa uchafuzi wa plastiki duniani, ambapo takriban tani milioni 430 za plastiki huzalishwa kila mwaka.

Karibu theluthi mbili ya taka hizo hutupwa tu, na kudhuru mazingira na mnyororo wa chakula.

Ikiitisha kikao chake cha tatu, Kamati ya Majadiliano ya Kiserikali INC-3 itazingatia kile kinachoitwa rasimu ya kutozalisha kabisa ya chombo cha kisheria cha kimataifa kuhusu uchafuzi wa plastiki, iliyotolewa mapema mwaka huu, kwa lengo la kuhitimisha mazungumzo kufikia mwisho wa 2024. 

Hasara katika uchumi ni kubwa

Kulingana na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya INC Jyoti Mathur-Filipp, athari mbaya za uchafuzi wa plastiki kwenye mifumo ya ikolojia, hali ya hewa, uchumi na afya ya binadamu, hugharimu sayari kati ya dola bilioni 300 na 600 kwa mwaka.

Uzalishaji wa plastiki unatarajiwa kuongezeka maradufu katika miaka 20 ijayo iwapo hatua hazitachukuliwa.

“Waandaaji wanadai mabadiliko ya kutoka kwa uchumi wa kutupa hadi uchumi wa kurejeleza".

INC-3 itakuwa na mikutano 12 ya kando kushughulikia masuala mbalimbali ya uchafuzi wa plastiki, ikiwa ni pamoja na uzalishaji na matumizi endelevu, mabadiliko ya mbinu ya kutumia vitu visivyo plastiki na zaidi.

Viongozi wanasisitiza haja ya kupunguza uzalishaji wa plastiki, kuondokana na matumizi ya mara moja na bidhaa za muda mfupi za plastiki, na kuhamia kwenye mbadala wa bidhaa zisizo za plastiki.

Nakala iko mezani

Katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya mazungumzo ya kina ya wiki hii ambayo wajumbe wanatumai yatakuwa makubaliano ya kimataifa, Rais wa INC Gustavo Meza-Cuadra Velasquez alisema "Tunaingia katika awamu muhimu sana ya mazungumzo yetu Kwa mara ya kwanza wanaingia kwenye majadiliano na maandishi."

Kikao kitaingia katika rasimu nyingine ya mijadala iliyopangwa kufanyika Aprili 2024 nchini Canada.

Wakati jumuiya ya kimataifa inapambana na mzozo wa uchafuzi wa plastiki, matokeo ya INC-3 yanaweza kuwa hatua muhimu mbele.

Nakala ya Rasimu ya kutozalisha kabisa ya chombo cha kisheria cha kimataifa, iliyotayarishwa na Mwenyekiti wa INC, kwa msaada wa Sekretarieti ya INC, sasa inapatikana katika lugha zote sita rasmi za Umoja wa Mataifa.