Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yasihi wadau kuangalia mtindo mpya wa ufadhili

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO Beth Bechdol akitembelea Kituo cha Usambazaji wa Virutubisho vya Dharura vya Mifugo huko Isiolo, Kenya. (Maktaba)
FAO/Luis Tato
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO Beth Bechdol akitembelea Kituo cha Usambazaji wa Virutubisho vya Dharura vya Mifugo huko Isiolo, Kenya. (Maktaba)

FAO yasihi wadau kuangalia mtindo mpya wa ufadhili

Msaada wa Kibinadamu

Takriban watu milioni 258 katika nchi na maeneo 58 ulimwenguni wanakabiliwa na njaa kali inayochochewa na migogoro ya silaha, majanga ya kiuchumi, mabadiliko ya tabianchi, umaskini na ukosefu wa usawa, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO na kutaka wadau kuangalia upya mtindo wa ufadhili.

Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO Bi. Beth Bechdol idadi inayoongezeka ya watu walioathiriwa kutokana na kuongezeka kwa migogoro ya kibinadamu katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro kama vile Ukanda wa Gaza, Ukraine, na Sudan, au walioathirika na mabadiliko ya tabianchi, inahitaji hatua za haraka na za pamoja ili kupatikana kwa suluhu. 

Akitolea mfano mzozo unaoendelea huko Sudan Bi. Bechdol amesema hali ya kutisha ya ukosefu wa chakula inaonesha wazi kwamba migogoro na njaa "vina uhusiano usioweza kutenganishwa."

“Tunaona karibu nusu ya wananchi wote wapo katika mazingira magumu ya uhaba wa chakula, karibu watu milioni 18 ambao wanatatizika. Kumekuwa na idadi kubwa ya watu kupoteza maisha. Watu wengi waliuawa, mamilioni ya watu waliuawa katika vita vya Sudan.”

Beth Bechdol ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, (FAO).
UN Geneva
Beth Bechdol ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, (FAO).

Naibu Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO amekumbusha kuwa ili kukabiliana na changamoto zinazoongezeka na za muda mrefu kama vile mabadiliko ya tabianchi ni lazima wadau kubonga bongo na kufikiria upya mtindo wa ufadhili wa kifedha. 

“Mizozo inaendelea kwa miaka mingi, mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa yanachukua muda mrefu miaka minane, miaka kumi, ukame, mafuriko ambayo yanaendelea kutokea. Kwa hiyo inatubidi kwa uangalifu, sote, kutafuta njia mpya za kufikiria juu ya uwiano sahihi, mbinu sahihi ya kujumuisha msaada kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wanawake katika majibu haya, kwa sababu nadhani kilimo ndicho kinachoweza kuwa kweli sehemu ya suluhisho la muda mrefu sio tu kufanyia kazi maswala yanayohusiana na njaa, lakini kama tunavyojua, hatimaye inafika mahali ambapo unajaribu sana kujenga ujasiri katika uchumi, maishani, katika hali ambazo ni matokeo ya hali hizi zote ngumu sana.”

​FAO imetoa ombi la dola bilioni 18 ili iweze kufanikisha usaidizi kwa kibinadamu kwa watu milioni 43 ili nao waweze kuzalisha chakula chao wenyewe kwa mwaka huu wa 2024.