Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yatoa dola milioni 12 kusaidia wananchi wa Sudan

Wanawake kutoka nchini Sudan wakitembea mahali salama Um Baru, Kaskazini mwa Darfur.
UNAMID/Hamid Abdulsalam
Wanawake kutoka nchini Sudan wakitembea mahali salama Um Baru, Kaskazini mwa Darfur.

FAO yatoa dola milioni 12 kusaidia wananchi wa Sudan

Msaada wa Kibinadamu

Juhudi zinazofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO za kusaka misaada kwa ajili ya wananchi wa Sudan wanaokabiliwa na njaa, ukame, na hali ngumu ya maisha ambayo kwa ujumla imechochewa na vita ya Ukraine zimezaa matunda baada ya mradi wao mpya kupata ufadhili wa dola milioni 12 kutoka Mfuko wa kukabiliana na dharura wa Umoja wa Mataifa CERF.

FAO imetangaza leo kupokea msaada huo wa fedha ambao utasaidia kaya laki moja na themanini elfu au wananchi laki 9 ambao ni wakulima, wafugaji kutoka kaunti 14 za nchi hiyo zilizoathirika zaidi, wakimbizi wa ndani, wakimbizi waliorejea, wakimbizi na wananchi wanaoishi katika maeneo ya vijijini.

Mwakilishi wa FAO nchini Sudan Babagana Ahmadu amesema  “Mchango huu wa ukarimu kutoka kwa CERF unamaanisha kuwa FAO inaweza kutoa kwa haraka pembejeo muhimu za kilimo kwa kaya za wakulima zilizo hatarini kabla ya msimu mkuu wa kilimo kuanza mwezi Juni. Itahakikisha kwamba wanaweza kuzalisha chakula cha kutosha kukidhi mahitaji yao kwa miezi ijayo.”

Takwimu za FAO zimebainisha kuwa takriban watu milioni 11 au asilimia 3 ya wananchi wa Sudan wanategemea msaada wa kibinadamu ili kuendesha maisha yao hii ikiwa ni idadi kubwa zaidi katika kipindi cha muongo mmoja.

Mradi huu uliopata ufadhili utatoa misaada ya kilimo na mifugo, ambayo inalenga kupunguza kwa haraka utegemezi wa msaada wa dharura wa chakula na kutoa suluhisho la muda mrefu, mfupi na wakati.

Wakulima watapatiwa mbegu zilizoidhinishwa za mazao, mikunde na mboga, jembe la punda na zana za mkono.

Wafugaji watapatiwa chanjo ya mifugo na dawa, malisho ya wanyama yenye protini nyingi, na kulamba madini. Pia watapatiwa mikokoteni ya punda na wanyama wenye tija.

Eneo jingine litakalo nufaisha wananchi ni kupatiwa fedha taslimu na ukarabati wa rasilimali za jamii kama vile miundombinu midogo ya maji, maeneo ya malisho na mengineyo yatakayo jitokeza kwa jamii husika.

Pamoja na ukweli kuwa ufadhili huu wa CERF umekuja kwa wakati na nimuhimu, bado FAO inahitaji haraka dola nyingine milioni 35 ili kuhakikisha zinafikisha msaada wa kutosha kwa kaya milioni mbili za wakulima na wafugaji walio katika mazingira magumu ili kuzalisha chakula chao wenyewe, kuweka mifugo yao hai na tija, kuimarisha ustahimilivu wao.