Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu zaidi ya 100,000 watawanywa na machafuko Cameroon:UNHCR

Mapigano ya wanajamii ncini Cameroon yamelazimu maelfu kukimbilia nchini CHAD
© UNHCR/Aristophane Ngargoune
Mapigano ya wanajamii ncini Cameroon yamelazimu maelfu kukimbilia nchini CHAD

Watu zaidi ya 100,000 watawanywa na machafuko Cameroon:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema mapigano kati ya jamii yaliyozuka huko Kaskazini mwa Cameroon katika kipindi cha wiki mbili zilizopita yamewafurusha takriban watu 100,000 kutoka makwao, na idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi. 

UNHCR inakadiria kuwa zaidi ya watu 85,000 wamekimbilia nchi jirani ya Chad, wakati takriban wananchi 15,000 wakisaka hifadhi ndani ya nchi yao.  

Shirika hilo limeeleza kwa sababu ufikiaji wa misaada katika eneo hilo ni mdogo huenda idadi ya watu waliotawanywa ikawa kubwa zaidi. 

Kwa mujibu wa shirika hilo la wakimbizi dalili zinaonyesha kuwa watu kutawanywa na kuingia nchini Chad kumeongezeka kwa kasi, kwani jumla ni karibu mara tatu ya idadi iliyoripotiwa wiki iliyopita, wakati watu 30,000 walikuwa wamevuka mpaka na kwenda kutafuta usalama.

Majeruhi wa mapigano hayo ya karibuni pia wameongezeka na kufikia watu 44 waliouawa na 111 kujeruhiwa, ikilinganishwa na wiki iliyopita ambapo waliofariki dunia walikuwa 22 na majeruhi 30. Kwa jumla, vijiji 112 vilichomwa moto. 

Waathirika wakubwa ni Watoto na wanawake 

UNHCR inasema idadi kubwa ya wanaowasili nchini Chad ni watoto, na asilimia 98 ya watu wazima ni wanawake.

Takriban watu 48,000 wamepata hifadhi katika maeneo 18 ya mijini huko N’Djamena, mji mkuu wa Chad, na watu 37,000 wametawanyika katika maeneo 10 ya mashambani kando ya ukingo wa Chad wa mto Logone. 

Pamoja na mamlaka, UNHCR, mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa na washirika wa kibinadamu wanaharakisha kutoa msaada wa kuokoa maisha. Shirika hilo limetangaza hali ya dharura ya ngazi ya 2 na linaongeza kwa kasi shughuli zake za kuwasaidia watu walioathirika nchini Cameroon na wakimbizi wapya walioingia nchini Chad.

Kwa mujibu wa shirika hilo wakimbizi wanahitaji sana makazi, mablanketi, mikeka na vifaa vya usafi.  

Baadhi wanakaribishwa kwa ukarimu na jumuiya za wenyeji, lakini wengi wao bado wanalala katika maeneo ya wazi na chini ya miti. 

UNHCR na Madaktari wasio na mipaka (MSF) wamesambaza kliniki zinazohamishika kwenye maeneo mengi ya wakimbizi.  

Uchunguzi wa kitabibu unaendelea na wagonjwa wanaohitaji msaada wa kiafya wanapewa rufaa kwenye vituo vya afya vya kitaifa.  

UNHCR, Shirika la msalaba mwekundu la Chad na Shirika la maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi, ambalo ni NGO ya Chad, wamekuwa wakitoa chakula cha moto katika maeneo yote ya wakimbizi. 

Zaidi ya hayo, timu zetu zinaisaidia Serikali kutambua maeneo mapya ya uhifadhi yaliyo karibu zaidi na mpaka ili kuwalinda vyema wakimbizi kulingana na viwango vya kimataifa. 

Huko Mbali Kaskazini mwa Cameroon, vikosi vya usalama vimetumwa na shughuli za kupokonya silaha zinaendelea.  

Ingawa matukio machache yameripotiwa katika wiki iliyopita, hali ya wasiwasi imesalia kuwa juu. 

Maelfu ya watu wamekimbia eneo la Kaskazini mwa Cameroon kwa kuvuka mito ya Chari na Logone ambayo inaashiria mpaka na Chad.
© UNHCR/Aristophane Ngargoune
Maelfu ya watu wamekimbia eneo la Kaskazini mwa Cameroon kwa kuvuka mito ya Chari na Logone ambayo inaashiria mpaka na Chad.

Bado kuna maeneo hayafikiki 

UNHCR bado haiwezi kufikia wilaya ya vijijini ya Logone Birni ambako mapigano yalianza, kutokana na ukosefu wa usalama.  

“Timu zetu katika miji ya Maroua na Kousseri zinatathmini ulinzi na mahitaji ya kibinadamu ya watu waliotawanywa ndani ya nchi. Wengi wa waliokimbia makazi yao wanaripoti matatizo ya kupata maji salama na hawana vyoo, na changamoto za masuala ya usafi zinaongezeka.” Limesema shirika hilo. 

Mapigano yalianza tarehe 5 Disemba katika kijiji cha mpakani cha Ouloumsa kufuatia mzozo kati ya wafugaji, wavuvi na wakulima kuhusu kupungua kwa rasilimali za maji.  

Mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi unazidisha ushindani wa rasilimali, hasa ya maji kwani kina katika ziwa Chad kimepungua kwa kiasi cha asilimia 95 katika miaka 60 iliyopita.

UNHCR na mamlaka za serikali ya Cameroon zimekuwa zikiongoza juhudi za upatanisho, zikiandaa kongamano mapema mwezi Desemba, ambapo wawakilishi wa jamii walijitolea kukomesha ghasia.  

“Lakini bila hatua za haraka za kushughulikia chanzo cha mzozo huo, hali inaweza kuongezeka kuwa mbaya zaidi.” Limeonya shirika la UNHCR

Pia shirika hilo linatoa wito wa kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa kuwasaidia waliolazimika kutawanywa na linasisitiza wito wake wa maridhiano ili kukomesha ghasia hizo ili watu waweze warudi nyumbani salama.