Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 123 zinahitajika kusaidia watu milioni 10.1 katika majimbo 17 yasiyo na uhakika wa chakula Sudan: FAO

Uwekezaji wa kigeni huambatana pia na teknolojia ambazo zinaweza kusaidia wajasiriamali wadogo kama Aisha Abdallah, kutoka jimbo la Kordofan Kaskazini nchini Sudan (Maktaba)
IFAD
Uwekezaji wa kigeni huambatana pia na teknolojia ambazo zinaweza kusaidia wajasiriamali wadogo kama Aisha Abdallah, kutoka jimbo la Kordofan Kaskazini nchini Sudan (Maktaba)

Dola milioni 123 zinahitajika kusaidia watu milioni 10.1 katika majimbo 17 yasiyo na uhakika wa chakula Sudan: FAO

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO leo limezingua mpango wa dharura wa kulinda na kurejesha uwezo wa kuishi kwa kutegemea kilimo wakati vita ikiendelea nchini Sudan.

Mpango huo wa dharura unaohitaji dola milioni 123 unalenga kusaidia kukabiliana na ongezeko la kutokuwa na uhakikia wa chakula nchini Sudan ambalo linaathiri watu milioni 10.1 katika majimbo 17, kwa kuwapa wakulima mbegu za dharura, vifaa vya matibabu ya mifugo na msaada katika sekta tiba ya mifugo na uvuvi.

Mpango huu ni muendelezo wa kazi ya FAO ya kushughulikia hali mbaya iliyokithiri inayosababishwa na mzozo unaoendelea kwenye jamii za wakulima wadogo, wafugaji na wavuvi. 

Pia unakamilisha kampeni ya dharura ya FAO ya usambazaji wa mbegu iliyokamilika hivi karibuni. 

Maghala ya WFP katika Bandari ya Sudan yanawekwa bidhaa za chakula kwa ajili ya usambazaji wa dharura.
© WFP/Mohamed Elamin
Maghala ya WFP katika Bandari ya Sudan yanawekwa bidhaa za chakula kwa ajili ya usambazaji wa dharura.

Mamilioni ya watu Sudan wanahaha kuishi

Mpango huo pia umewasaidia wakulima kuongeza uzalishaji wa nafaka, kuepuka kupungua kwa mali na kuchagiza matumizi mseto ya mbegu na uzalishaji unaotarajiwa utachangia kukidhi mahitaji ya nafaka ya angalau watu milioni 13 na hadi watu milioni 19 kwa msimu ujao wa mavuno wa 2023.

Hongjie Yang, mwakilishi wa FAO nchini Sudan amesema, "mamilioni ya watu kote nchini Sudan wanakabiliwa na mgogoro wa kuweza kuishi huku changamoto ya kutokuwa na uhakika wa chakula ikizidi kuwa mbaya. Mpango huu wa kukabiliana na dharura unalenga kuzipa familia za wakulima, wafugaji na wavuvi mambo ya msingi wanayohitaji ili kuendeleza uzalishaji na kujilisha wao wenyewe na jamii zao."

Kampeni ya kugawa mbegu, na chanjo za wanyama na mifugo

Chini ya mpango huo, wa kusaidia jumla ya watu milioni 10.1, kaya zenye uhitaji zaidi zitapokea mbegu bora zilizoidhinishwa za kunde, karanga, ulezi, bamia na mtama kwa msimu wa kiangazi wa 2024, na kunde, matango, mbaazi, nyanya na matikiti maji kwa msimu wa baridi wa 2023. 

Pia watapata mafunzo ya kufuata kanuni bora za kilimo, kama vile utunzaji bora wa bidhaa za shambani baada ya mavuno.

Watu wanaoishi katika mazingira magumu ambao wamepoteza uwezo wao wa uzalishaji watasaidiwa kupitia uhifadhi wa mifugo. 

Hii itachangia uboreshaji wa haraka wa uhakika wa chakula na lishe na kuwezesha wafugaji kuzalisha lita 4 hadi 5 za maziwa kwa siku.

Kimsingi, katika mazingira ya mgogoro unaoendelea , mpango wa FAO utasaidia utekelezaji wa kampeni kubwa ya chanjo ya kulinda kondoo, mbuzi na ng'ombe milioni 6 dhidi ya magonjwa yaliyoenea na mabaya, ikiwa ni pamoja na wanyama kucheua, wadudu waharibifu, na ugonjwa unaoathiri miguu na midomo kwa kondoo na mbuzi.