Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yaisaidia DRC katika mafuriko mabaya kuhushudiwa kwa miaka 60

Mtoto mdogo akipokea matibabu katika kituo cha matibabu ya kipindupindu huko Kivu Kaskazini, DR Congo.
© UNICEF/Jospin Benekire
Mtoto mdogo akipokea matibabu katika kituo cha matibabu ya kipindupindu huko Kivu Kaskazini, DR Congo.

UNICEF yaisaidia DRC katika mafuriko mabaya kuhushudiwa kwa miaka 60

Tabianchi na mazingira

Mjini Kinshasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na wadau wengine wa misaada ya kibinadamu wamesema wanafanya kila liwezekanalo kuwasaidia waathirika wa mafuriko mabaya zaidi nchini humo yaliyosababisha kina cha mto Congo kufurika katika kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha zaidi ya miaka 60.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA majimbo 18 kati ya 26 ya DRC yameathirika na mafuriko hayo na kuwaacha watu zaidi ya milioni 2.2 ambapo karibu asilimia 60 ni watoto wakihitaji msaada wa kibinadamu. Mafuriko hayo pia yameharibu kaya 100,000, shule 1325, na vituo vya afya 276.

Pia yameharibu mazao na mashamba hali inayoashiria kutokea kwa upungufu mkubwa wa chakula katika baadhi ya maeneo.

UNICEF inasema wakati asilimia 40 ya wagonjwa wa kipindupindu wako katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo inaongeza juhudi kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo.

Kumekuwa na mafuriko makubwa kupindukia mjini Kinshasa baada ya Mto Congo kupanda hadi kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha zaidi ya miaka sitini.
© UNICEF/Josue Mulala
Kumekuwa na mafuriko makubwa kupindukia mjini Kinshasa baada ya Mto Congo kupanda hadi kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha zaidi ya miaka sitini.

Mvua zaidi zinatarajiwa

Kwa mujibu wa UNICEF utabiri wa hali ya hewa unaonya juu ya mvua nyingi zaidi kunyesha, na kuongeza uwezekano kwamba kipindupindu kitasafiri kutoka maeneo ambayo ni janga kupitia mto Congo hadi katikati mwa jiji la Kisangani na kisha hadi Kinshasa, mji mkuu wa DRC. 

Katika hali kama hiyo mwaka 2017, kipindupindu kilienea hadi nchi nzima, na kusababisha karibu wagonjwa 55,000 na zaidi ya vifo 1,100.

"Watoto nchini DRC wanakabiliwa na mafuriko mabaya zaidi kuwahi kutokea katika miongo kadhaa na mlipuko mbaya zaidi wa kipindupindu kuwahi kutokea katika miaka mingi. Maji yanayoongezeka yanaharibu nyumba zao na kuongeza tishio la magonjwa yanayosambazwa na maji, hivyo kuwaweka katika hatari kubwa zaidi,” amesema mwakilishi wa UNICEF nchini DRC, Grant Leaity. 

Ameongeza kuwa "Bila hatua za haraka za kutoa maji salama, usafi wa mazingira, na huduma za afya ili kudhibiti kuenea kwa kipindupindu, mafuriko yaliyoenea yanaweza kusukuma idadi ya wagonjwa katika viwango visivyo na kifani."

Na mwaka 2023, zaidi ya visa 52,400 vya kipindupindu na vifo 462 vilirekodiwa nchini DRC, na kuifanya kuwa moja ya milipuko mikubwa zaidi ulimwenguni, kulingana na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO

DRC ilichangia asilimia 80 ya visa vyote vya kipindupindu katika Afrika Magharibi na Kati.

Mfanyakazi wa jumuiya anaelimisha familia katika eneo la wakimbizi wa ndani huko Kivu Kaskazini, DR Congo kuhusu mazoea mazuri ya kukabiliana na kipindupindu.
© UNICEF/Jospin Benekire
Mfanyakazi wa jumuiya anaelimisha familia katika eneo la wakimbizi wa ndani huko Kivu Kaskazini, DR Congo kuhusu mazoea mazuri ya kukabiliana na kipindupindu.

Msaada unaotolewa na UNICEF

UNICEF inatoa msaada wa maji ya kunywa, tembe za kusafisha maji, na vifaa vya afya kwa maeneo yaliyoathirika. 

Shirika hilo pia linafanya kazi na mamlaka za mitaa ili kuhakikisha kuendelea kwa huduma za ulinzi wa watoto, kama vile kuwaunganisha watoto waliotenganishwa na familia zao na kutoa msaada wa afya ya akili.

Timu za kudhibiti kipindupindu zinazoungwa mkono na UNICEF pia ziko mashinani, na kutoa huduma ya kwanza wakati visa vya kipindupindu vinashukiwa. 

Hii ni pamoja na kusambaza vifaa vya kuzuia kipindupindu, kusafisha nyumba na vyoo vya jumuiya, na kuweka vituo vya kuua vijidudu kwa kutakasa mikono. 

Vikundi hivyo pia vinaongeza hatua za kuzuia, ikiwa ni pamoja na juhudi za uhamasishaji na ufuatiliaji, na kuboresha vituo vya matibabu ya kipindupindu, ikiwa ni pamoja na katika mji mkuu Kinshasa.

Ili kuunga mkono mpango wa serikali wa kukabiliana na mafuriko, UNICEF inatumia ufadhili wa msingi wa dola 700,000 kuanzisha msaada wa huduma za WASH, afya na ulinzi wa watoto. 

Jumla ya dola milioni 9 zinahitajika kwa ajili ya hatua za awali za UNICEF kukabiliana na mafuriko katika maeneo matatu yaliyoathirika zaidi.