Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 490,000 wameathirika na mafuriko Sudan Kusini:UNICEF

Mvua kubwa nchini Sudan Kusini zimesababisha mafuriko kwenye kambi za wakimbizi kwenye kaunti ya Maban nchini humo
© UNHCR/Elizabeth Stuart
Mvua kubwa nchini Sudan Kusini zimesababisha mafuriko kwenye kambi za wakimbizi kwenye kaunti ya Maban nchini humo

Watoto 490,000 wameathirika na mafuriko Sudan Kusini:UNICEF

Tabianchi na mazingira

Watoto takriban 490,000 wameathirika na mafuriko makubwa nchini Sudan Kusini limeonya leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF na kuongeza kuwa mvua kubwa zilizoanza kunyesha tangu mwezi Julai mwaka huu zimeathiri jumla ya watu 908,000 katika kaunti 32.

UNICEF inasema ingawa mvua kubwa na mafuriko ni kitu cha kawaida nchini humo kwa msimu kama huu lakini yam waka huu yamefurutu ada hasa katika majimbo ya amani ya Jonglei, Upper Nile, Warrap na jimbo la Kaskazini la Bahr El Ghazal. Na mvua bado zinatarajiwa kuendelea kunyesha kwa wiki zingine nne.

Athari za mafuriko hayo

Kwa mushibu wa shirika la UNICEF mafuriko hayo yameathiri sehemu nyingi za nchi hiyo, vituo kadhaa vya afya vimefurika maji na haviwezi kutoa huduma zozote kwa watu. Na kwa baadhi ya vituo vya afya ambavyo viko wazi vingine havifikiki na Watoto wewngi na familia zao kutokana na barabara kujaa maji na kutopitika  na pia kuharibiwa kwa madaraja. Cha kuskitisha Zaidi limesema shirika hilo tayari huduma za afya zilikuwa katika hatihati hata kabla ya mafuriko na sasa kutokana na changamoto za fursa ya kufikia vituo hivyo  mlipuko wa malaria na ugonjwa wa kuhara katika maeneo haya umefanya hali kubwa mbaya zaidi inayohitaji hatua za haraka kunusuru Maisha ya wengi. “Nchini Sudan Kusini maji kwa kawaida huusishwa na uhai , lakini sasa maji yanaweka Maisha ya Watoto katika hatari kubwa. UNICEF ina hofu kubwa kuhusu afya ya Watoto katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko  kukiwa na ongezeko la na magonjwa ya malaria na mengine yanayosababishwa na maji kama kuhara ambayo ni magonjwa mawili yanayoua sana Watoto Sudan Kusini.” Amesema mwakilishi wa UNICEF nchini humo Dkt.Mohamed Ag Ayoya.


Mafuriko yamechafua vyanzo vya maji na familia 70,000 zimetawanywa kwa muda kutokana na nyumba zao kuzama na mafuriko. Shule zimefungwa baada ya kujaa maji na baadhi ya mdarasa kutumika kama malazi kwa watu waliotawanywa na mafuriko hayo na kusababisha maelfu ya Watoto kutohudhuria shule.

Hali halisi

Asilimia 60 ya kaunti zilizoathirika na mafuriko zina viwango vikubwa vya utapiamlo hata kabla ya mvua kuanza kunyesha hivyo mafuriko haya yanaweza kuongeza kiwango cha utapiamlo miongoni mwa watotokutokana na kiwango kikubwa cha malaria, kutopata maji safi na masuala ya usafi. “Vituo 42 vya lishe vimesitisha huduma kutokana na mafuriko hali ambayo itaweza kuzidisha hali ya utapiamlo ambayo tayari ilikuwa mbaya kuwa mbaya Zaidi na vifo ni moja ya matokeo ya hali hiyo endapo Watoto hawatotibiwa kwa wakati.”

UNICEF inasema endapo msaada hautotolewa kwa wakati basi athari za mafuriko hayo zitaenda mbali Zaidi ya wakati ambapo maji yatatuama. Hivi sasa maeneo mengi ya kilimo na malisho ya mifugo yamefunikwa na maji hii itasababisha ugumu wa upatikanaji wa chakula kwa Watoto na familia zao. Na hii itaathiri zaidi hali ya chakula ambayo tayari ilikuwa mbaya na waathirika wakubwa watakuwa ni Watoto. Kwa hali ya sasa shirika hilo linasema shule zitahitaji kujengwa upya na kampeni ya uandikishaji Watoto shule inahitajika ili Watoto waweze kurejea madarasani.

UNICEF inafanyakazi na serikali ya Sudan kusini na wadau wengine ili kukabiliana na mafuriko hayo na athari zake na inaomba dola milioni 5.5 kuweza kukidhi mahitaji ya haraka ya Watoto katika maeneo yaliyoathirika zaidi za mafuriko.