Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa ufupi: Msaada wa kibinadamu Gaza; Wandishi wa Habari; Saratani

Timu za UNRWA zinaendelea kusambaza misaada ya kibinadamu huko Gaza.
© UNRWA
Timu za UNRWA zinaendelea kusambaza misaada ya kibinadamu huko Gaza.

Habari kwa ufupi: Msaada wa kibinadamu Gaza; Wandishi wa Habari; Saratani

Msaada wa Kibinadamu

Kufuatia uamuzi wa nchi 16 wafadhili kusitisha utoaji fedha kwa shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi wa kipalestina UNRWA baada ya Israel kulishutumu shirika hilo kuwa wafanyakazi wake 12 walihusika katika shambulio lililotokea tarehe 7 Oktoba mwaka jana, Mkuu wa UNRWA Philipe Lazzarini amesema kuwa iwapo fedha zitaendelea kuzuiliwa, watalazimika kufunga operesheni zao ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Februari. 

UNRWA yenye wafanyakazi zaidi ya 13,000 ndio shirika kubwa zaidi la misaada huko Gaza linalohudumia zaidi wa wapalestina milioni 2 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto. 

Mauaji ya waandishi wa habari

Wataalamu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameeleza kusitikishwa na kulaani vitendo vya waandishi wa habari kuuawa, kushambuliwa, kujeruhiwa na kuwekwa vizuizini huko katika eneo la palestina linalokaliwa kwa mabavu na kutoa wito kwa pande zote kwenye mzozo kuhakikisha wanalinda waandishi wa habari. 

Katika taarifa yao kutoka Geneva Uswisi hii leo wataalamu hao wameeleza kupokea ripoti zakusikitisha kwamba licha ya waandishi wa habari kuvaa majaketi, kofia na kuwa kwenye magari ya kuwatambulisha kuwa wao ni vyombo vya habari lakini bado walishambuliwa na kuuawa kitendo ambacho wanaeleza kinaonekana kuwa ni mkakati wa makusudi wa vikosi vya Israel kuzuia vyombo vya habari na kunyamazisha kutolewa kwa ripoti muhimu.

Saratani

Tumalizie na masuala ya afya ambapo Shirika la kimataifa la utafiti wa saratani, IARC ambalo ni shirika tanzu la WHO hii leo limetangaza matokeo ya utafiti wake uliofanyika katika nchi 115 wakiangazia mzigo wa kimataifa wa saratani ambapo wamebaini kuwa nchi nyingi hazitoi kipaumbele na kufadhili ipasavyo huduma za matibabu ya saratani kama sehemu ya mpango wa afya kwa wote. 

Utafiti huo uliofanyika mwaka 20222 umeonesha kuongezeka kwa mzigo wa ugonjwa wa saratani hususan katika jamii za watu wasio na uwezo na kuonesha hitaji la dharura la kushughulikia ukosefu wa usawa wa saratani ulimwenguni.