Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa ufupi: Gaza; Sudan; Watoto Ulaya na Asia ya kati

Malori yaliyosheheni msaada wa kibinadamu yakijiandaa kuingia Gaza kupitia kivuko cha Rafah. (Maktaba)
© UNICEF/Eyad El Baba
Malori yaliyosheheni msaada wa kibinadamu yakijiandaa kuingia Gaza kupitia kivuko cha Rafah. (Maktaba)

Habari kwa ufupi: Gaza; Sudan; Watoto Ulaya na Asia ya kati

Amani na Usalama

Hii leao mashirika ya Umoja wa Mataifa yamerejea kupaza sauti kuhusu misaada muhimu ya kibinadamu kuendelea kuruhusiwa kuingia Gaza, lile la kuratibu Misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA likisema kwa mara ya kwanza dawa kwa ajili ya mateka wa Israel zimeripotiwa kuruhusiwa kuingia leo sanjari na msaada kwa ajili ya Wapalestina kwa makubaliano maalum yaliyowezeshwa na serikali za Qatar na Ufaransa.

Lile la kuhudumia Watoto UNICEF kupitia naibu mkurugenzi mtendaji wake Ted Chaiban ambaye amehitimisha ziara Ukanda wa Gaza limesema hali inatoka kuwa janga kuelekea kuwa zahma kubwa na kulifanya eneo hilo kuwa mahala pa hatari Zaidi kuishi duniani kwa Watoto.

Na la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limeonya kuhusu ongezeko la watu wanaokimbilia Kusini mwa Gaza hasa Rafah kuwa idadi yao imeongezeka mara nne na sasa kufikia watu milioni 1.2 wengi wakihaha kugombea huduma zisizotosheleza za chakula, malazi yaliyofurika na dawa.

Watoto na familia wakikimbia kwa miguu kutoka Wad Madani, jimbo la Al Jazirah kufuatia mapigano ya hivi karibuni.
© UNICEF/UNI492302/Mohamdeen
Watoto na familia wakikimbia kwa miguu kutoka Wad Madani, jimbo la Al Jazirah kufuatia mapigano ya hivi karibuni.

Vita Sudan

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kutafuta ukweli nchini Sudan umeanza kazi yake kwa ujumbe wa awali kuwasili mjini Geneva wiki hii, ukizitaka pande zinazozozana Sudan kumaliza vita, kutekeleza wajibu wao wa kulinda raia na kuhakikisha kwamba wahusika wa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na uhalifu wanawajibishwa.

Akizungumza baada ya siku kadhaa za mazungumzo na viongozi na mashirika ya kiraia nchini Sudan, Mohamed Chande Othman, ambaye ni mwenyekiti wa ujumbe huo wa kuutafuta ukweli, amesema leo kwamba uchunguzi kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu unaendelea.

Benaziz mwenye umri wa miaka 30, akiwa na watoto wake kwenye kijiji cha Balocho Zardari huko jimboni Sindh.
© UNICEF/Juan Haro
Benaziz mwenye umri wa miaka 30, akiwa na watoto wake kwenye kijiji cha Balocho Zardari huko jimboni Sindh.

Ulaya na Asia ya kati                                          

Barani Ulaya ripoti mpya iliyochapishwa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF inasema takriban watoto nusu milioni kote barani Ulaya na Asia ya Kati wanaishi katika vituo vya makazi ya kulelea watoto pamoja na katika taasisi kubwa.

Shirika hilo linasema idadi hiyo ni mara mbili ya wastani wa kimataifa, kwani watoto 232 kati ya kila watoto 100,000 wakiishi katika makazi ya vituo hivyo ikilinganishwa na kila Watoto 105 kati ya 100,000 kwingineko duniani kote.

Regina De Dominicis, (TAMKA DIDOMINIKIS) Mkurugenzi wa UNICEF baran Ulaya na Asia ya Kati ameoinya kwamba “Bado kuna safari ndefu na ya machungu kabla ya kufanikiwa kukomesha hali hiyoi iliyokita mizizi ya kuwalea watoto katika vituo Ulaya na Asia ya Kati.”