Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita Sudan ni jinamizi kwa watoto: Mwakilishi wa UNICEF

Watoto waliokimbia makazi yao kutokana na vita nchini Sudan sasa wanaishi Atbara.
© UNICEF/Abdulazeem Mohamed
Watoto waliokimbia makazi yao kutokana na vita nchini Sudan sasa wanaishi Atbara.

Vita Sudan ni jinamizi kwa watoto: Mwakilishi wa UNICEF

Amani na Usalama

Vita nchini Sudan vinahatarisha mustakabali wa raia wake milioni 24 wenye umri mdogo zaidi, ameonya Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF nchini humo.

Mandeep O’Brien ameyasema hayo wiki hii katika mahojiano maalum na UN News na kuongeza kuwa "Sudan inakabiliwa na janga kubwa la kibinadamu lisiloelezeka. Ni jinamizi lililo hai kwa watoto.” 

Takriban miezi 10 imepita tangu mapigano yalipozuka kati ya Jeshi la Sudan SAF na kundi pinzani la msaada wa haraka RSF, na kusababisha watoto milioni 14 kukihitaji msaada wa kuokoa maisha.

Mvuana akitembea katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al Salaam Darfur Kaskazini
© WFP/Leni Kinzli
Mvuana akitembea katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al Salaam Darfur Kaskazini

Mgogoro wa kutawanywa kwa watoto

Bi O’Brien amesema mapigano hayo yamesababisha mgogoro mkubwa zaidi wa watoto kutawanywa duniani. 

Zaidi ya wavulana na wasichana milioni 3.5 wamekimbia makazi yao na kwenda kutafuta maeneo salama, huku wengine wakilazimika kukimbia mara kadhaa.

Habari mbaya zinaendelea kwani zaidi ya vijana milioni 7.4 wa Sudan hawana maji safi ya kunywa, jambo linalowaweka katika hatari ya magonjwa yatokanayo na maji, na karibu milioni mbili wanahitaji chanjo ya dharura ya kuokoa maisha.

Bi O’Brien pia amesema “Sudan ina moja ya viwango vya juu zaidi vya utapiamlo wa watoto ulimwenguni. Zaidi ya watoto milioni tatu wa chini ya umri wa miaka mitano wanakabiliwa na utapiamlo mkali, na 700,000 wanaweza kufa kutokana na hali mbaya zaidi endapo hawatapatiwa matibabu.”

Kupata elimu ni mtihani mkubwa

Zaidi ya hayo, amesema watoto milioni 19 wenye umri wa kwenda shule hawako darasani, na hivyo kuweka Sudan katika hatari ya kuwa mojawapo ya matatizo mabaya zaidi ya elimu duniani.

Ameongeza kuwa hebu "Fikiria mustakabali wa nchi hii ikiwa watoto hawawezi kusoma. Tunakadiria kuwa ikiwa hali hii itaendelea, Sudan itakuwa inakabiliwa na hasara ya maisha ya dola bilioni 26."

Bi. O’Brien amesema elimu ni chombo chenye nguvu ya kujenga amani "kwa sababu watoto wanapokuwa darasani, wanahisi salama, wamelindwa, na wanaweza kuishi pamoja kwa amani. Haya ni maadili ambayo hatupaswi kuyachukulia kirahisi. Haya ni maadili ambayo watoto wanapaswa kuyaishi na kuyatekeleza.”

Watoto wakichora mapicha kwenye nafasi inayofadhiliwa na UNICEF katika kambi iliyoko Darfur Kusini, Sudan, kwa watu waliokimbia makazi yao kutokana na vita. (Maktaba)
© UNICEF/Adriana Zehbrauskas
Watoto wakichora mapicha kwenye nafasi inayofadhiliwa na UNICEF katika kambi iliyoko Darfur Kusini, Sudan, kwa watu waliokimbia makazi yao kutokana na vita. (Maktaba)

Shule zinfunguliwe na waalimu walipwe 

UNICEF imekuwa ikishinikiza mamlaka ya shirikisho na serikali ya Sudan kufungua tena shule, lakini Bi O’Brien ametaja kikwazo kingine cha elimu.

"Ili hilo lifanyike, walimu wanahitaji kulipwa. Cha kusikitisha, tangu kuanza kwa vita hivi, walimu na wafanyikazi wengine walio mstari wa mbele hawajalipwa mishahara yao, kwa hivyo hii lazima ifanyike."

Kwa muda mfupi, UNICEF na washirika wake wamekuwa wakitafuta suluhisho la vitendo na njia za kusaidia ufunguaji upya kwa usalama wa shule pale ambapo masharti yanaruhusu, huku pia wakifanya kazi kuwafikia wanafunzi wadogo zaidi.

Kupanua wigo wa kujifunza

"Idadi kubwa ya watoto ambao hawawezi kwenda shule, ambao hawakusajiliwa au kuandikishwa shuleni kabla ya vita, tunajaribu kuleta watoto wengi iwezekanavyo katika wigo mpana wa kujifunza, kwa kutumia njia mbadala za kujifunza," amesema. 

Ili kushughulikia mahitaji yao, UNICEF na washirika wamezindua maeneo rafiki kwa watoto katika maeneo ya makazi ya wakimbizi wa ndani.

Yakijulikana kama Makanna kwa Kiarabu yakimaanisha "Mahali Petu" haya ni maeneo ambapo watoto wanaweza kujisikia salama na kulindwa huku pia wakiendelea na masomo kupitia mtandao au e-learning na kujaribu suluhisho za kidijitali za gharama nafuu.

Zaidi ya Makanna 850 yamesambazwa kote Sudan, na kufikia zaidi ya watoto 250,000 ambao pia wanapata usaidizi wa kisaikolojia ili kukabiliana na kiwewe kilichotokana na vita.

Tarehe 7 Juni 2023, kikundi cha watoto kutoka katika kituo cha watoto yatima cha Mygoma huko Khartoum walifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na wafanyakazi wa afya wakiwemo maafisa wa afya wa UNICEF huko Madani. Watoto hao wako chini ya uangalizi wa wizara …
© UNICEF/UN0854045/
Tarehe 7 Juni 2023, kikundi cha watoto kutoka katika kituo cha watoto yatima cha Mygoma huko Khartoum walifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na wafanyakazi wa afya wakiwemo maafisa wa afya wa UNICEF huko Madani. Watoto hao wako chini ya uangalizi wa wizara ya Ustawi wa Jamii na Afya, huku UNICEF ikisaidia matibabu ya watoto, kuwalisha, kuwachangamsha kisaikolojia, michezo na shughuli za elimu, na kusaidia walezi kwa watoto waliohamishwa. Mandeep O'Brien, Mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan.

Kampeni za chanjo

Bi O’Brien  amesema mzozo huo pia umenyoosha mfumo wa afya wa Sudan hadi kikomo. 

UNICEF pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO na washirika wake wanaendelea kushirikiana na mamlaka kutoa huduma zinazohitajika haraka huku kukiwa na milipuko ya magonjwa, pamoja na kufanya kampeni za chanjo ya watoto.

Ameongeza kuwa hadi sasa wamewachanja zaidi ya watoto milioni moja dhidi ya surua “jambo ambalo linatia wasiwasi mkubwa na kwa sasa linaenea tunapozungumza.”

Wiki hii ilikuwa mwanzo wa kampeni ya kukabiliana na surua na rubela, iliyozinduliwa kwa msaada wa Muungano wa Kimataifa wa Chanjo GAVI. 

Lengo ni kutoa chanjo kwa watoto zaidi ya milioni tano katika majimbo saba ifikapo mwisho wa wiki na milioni 15 katika miezi ijayo.

Sabuni inasambazwa katika mji wa Gedaref, mashariki mwa Sudan, ili kusaidia unawaji mikono wakati wa mlipuko wa kipindupindu.
© UNICEF/Omar Tarig
Sabuni inasambazwa katika mji wa Gedaref, mashariki mwa Sudan, ili kusaidia unawaji mikono wakati wa mlipuko wa kipindupindu.

Wito wa amani

Ingawa akihofia kuwa Sudan inaweza kukabiliwa na hatari ya kuwa mzozo uliosahaulika wakati mzozo ukiendelea huko Gaza na kuzidi kushika kasi wa nchini Ukraine, Bi O’Brien amesisitiza dhamira ya UNICEF ya kusalia na kutoa huduma madhubuti pamoja na washirika wake.

Mwaka jana, walifikia zaidi ya watoto na familia milioni 6.4 kwa vifaa vya afya vinavyohitajika haraka na kuwapima zaidi ya watoto milioni tano wenye umri wa chini ya miaka mitano magonjwa ya utapiamlo, na kutibu zaidi ya kesi 300,000 mbaya zaidi.

Ameomba ufadhili zaidi ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya watoto, wanawake na familia.

"Muhimu zaidi ni kwamba tunahitaji juhudi zote za kimataifa na kikanda kuunganishwa ili Sudan iweze kupata suluhu ya kisiasa kwa janga hili” amesema akiongeza kuwa "Vita hivi lazima vikome sasa. Sudan inahitaji amani sana.”