Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ECW watoa ruzuku ya dola mil 5 kwa Sudan kusaidia elimu

Wavulana watano wadogo, ambao huenda ni watoto waliohamishwa, wamesimama katika eneo lenye vumbi nje huko Atbara, Sudan. Wameshikilia au wamesimama karibu na vyombo vikubwa vya maji vya plastiki.
© UNICEF/Abdulazeem Mohamed Watoto waliokimbia makazi yao kutokana na vita nchini Sudan sasa wanaishi Atbara.

ECW watoa ruzuku ya dola mil 5 kwa Sudan kusaidia elimu

Utamaduni na Elimu

Mfuko wa kimatifa wa elimu haiwezi kusubiri ECW umetangaza kutoa ruzuku ya dola milioni 5 kusaidia wanafunzi 86,000 nchini Sudan ambao kwa sasa wanashuhudia athari za vita inayoendelea nchini mwao. 

Mkurugenzi Mkuu wa ECW Yasmine Sherif katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa leo jijini New York Marekani amesema fedha hizo zitakabidhiwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto UNICEF pamoja na shirika la Save the children ambayo kwa pamoja wataweza kuwahudumia watoto wa majimbo mawili West Darfur na White Nile kwa kipindi cha miezi 12. 

Bi.Sherif anasema watoto wa Sudan wameteseka sana “Watoto wameuawa, wamepoteza wanafamilia, wamelazimika kukimbia nyumba zao katika mazingira magumu zaidi na kuona elimu yao ikikatizwa ghafla. Mgogoro huu unasambaratisha huduma za msingi za kijamii nchini Sudan - huku watoto wenye umri wa kwenda shule na walimu wao wakilipa gharama kubwa zaidi.

ECW inaamini kwa watoto kupata fursa za elimu ya kuokoa maisha, zinasaidia kuwalinda wasichana na wavulana dhidi ya janga la ukatili, ndoa za utotoni, kulazimishwa kujiunga na vikundi vya wapiganaji wenye silaha, unyonyaji na unyanyasaji. 

Yasmine Sherif, Mkurugenzi wa Elimu Cannot Wait, anazungumza wakati wa mahojiano akiwa na mandhari ya bluu.
UN News Mkurugenzi Mkuu wa ECW Yasmine Sherif

Fedha zitatumikaje?

Ruzuku hiyo ya dola milioni 5 inalenga katika kuboresha upatikanaji wa elimu bora, jumuishi, inayozingatia jinsia na elimu rafiki kwa mtoto. 

Kwa kuwapatia elimu watoto wa majimbo hayo mawili wanatarajia watachangia kwa watoto kufikia matokeo bora ya kujifunza kupitia usaidizi kwenye vituo vya kujifunzia. 

Fedha hizo si kwa wanafunzi pekee bali pia zitahakikisha walimu wanapata mafunzo, zana na motisha ya kufanya kazi zao na kutoa ufikiaji wa kuokoa maisha wa usaidizi wa elimu ya jumla ili kuhakikisha ulinzi na ustawi wa watoto.

Ruzuku hiyo inatarajiwa kutoa elimu bora kwa kiwango vya juu na kwa kasi, ufanisi na ushirikiano wa kiutendaji. 

Hata hivyo, pengo kubwa la ufadhili linaendelea kusalia nchini humo kwani makadirio ya hivi karibuni yakionesha angalau dola milioni 40 zitahitajika kuongeza elimu ya kuokoa maisha katika kukabiliana na dharura nchini Sudan.

Kusoma zaidi kuhusu ruzuku hii bofya hapa.