Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je wajua  kwamba watoto Rwanda wanaanza kupokea chanjo zao za kawaida karibu na nyumbani?

Mtoto akipokea chanjo. (Maktaba)
© UNICEF
Mtoto akipokea chanjo. (Maktaba)

Je wajua  kwamba watoto Rwanda wanaanza kupokea chanjo zao za kawaida karibu na nyumbani?

Afya

Madhari inayoundwa na vilima 1000 kote nchini Rwanda ni ya kupendeza lakini kwa kipindi Fulani kutoka na huduma za afya kuwa mbali, ilikuwa ni shughuli pevu ya panda shuka kuifuata huduma hiyo katika umbali mrefu.

Esperance Habuhaze ni mkazi wa Rubavu, moja ya wilaya za Jimbo la Magharibi mwa Rwanda anasema hivi sasa ana watoto watano. Kila wakati wa chanjo za watoto alikuwa anapata changamoto. Umbali kutoka nyumbani hadi vituo vya chanjo ulikuwa mrefu. Anaeleza kwamba wakati mwingine alikuwa anakosa kufika kwenye chanjo kwasababu ya kukosa usafiri. Anaendelea kueleza kwamba ni takribani saa tatu kwa mwendo wa miguu au gharama ya faranga 2500 za Rwanda sawa na takribani dola mbili za kimarekani kwa usafiri wa pikipiki. 

Lakini sasa hali ni tofauti na Esperance anasema licha ya afya pia miradi hii ya UNICEF imekuwa na msaada mkubwa hata kiuchumi, 

“Tunashukuru kwamba huduma hii ya chanjo sasa iko karibu na makazi yetu. Changamoto tulizokuwa nazo sasa zimeisha. Hivi sasa ile hela niliyokuwa ninaitumia kusafiria ninaitumia kununua matumizi ya nyumbani na vitu vingine muhimu vya nyumbani. Kabla muda wetu mwingi wa uzalishaji ungetumika katika kusafiri kwenda kwenye kvituo vya afya. Sasa tunaweza kufanya kazi zaidi kwa kuwa tunaokoa muda kwa kuwa chanjo inatumia kama dakika 10 hadi 20.”

UNICEF kwa kushirikiana na wadau kama Ubia wa Chanjo Duniani (GAVI), Shirika la Marekani la misaada kwa maendeleo ya kimataifa (USAID) na Rwanda Biomedical Centre siyo tu wameweza vituo vya afya kujengwa karibu na makazi ya watu, bali pia wamesaidia vituo kuwa na teknolojia ya kuweka kumbukumbu vizuri na kurahisisha kufuatilia wanaostahili huduma. Dusabimana Ruth ni mkuu wa Kituo cha Afya cha Gora huko hukoRubavu anasema, 

“Kuna wakati watu walikuwa wanakosa chanjo wakati walipokuwa wanakuwa wanakuwa wengi katika kituo cha afya au wakati mtu wa kuchanja hakuwepo. Lakini sasa chanjo itakuwa inapatikana kama ilivyopangwa kwasababu watu wanazingatia miadi yao na hata wanapokosa, ufuatiliaji unakuwa rahisi. Tunaweza sasa kuwatambuawatoto ambao wamekosa miadi ya chanjo kwasababu tunahifadhi kidijitali kumbukumbu za wale wanaofika na ni lini wamepangiwa kurejea kwa ajili ya mzunguko unaofuata. Wanapokosa kufika tunafuatilia kuhakikisha wanachanjwa kwa wakati.”

Twizerimana Marie Louise ni Mkuu wa Kituo cha Afya cha Gakoro katika Wilaya ya Musanze, katika Jimbo la kaskazini mwa Rwanda anasema,

“Mafunzo haya yanahusu uchanjaji wa watoto. Tunapata mengi kutoka kwenye mafunzo haya kwasababu vituo vya afya vinapokea idadi kubwa kutoka katika jamii. Ni thamani kubwa kwetu kwamba chanjo zimeongezwa katika huduma za msingi za vituo.”