Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFPA ilivyorejesha matumaini ya wanawake na wasichana wa Darfur Magharibi Sudan

Mwanamke akipokea matibabu katika kliniki ya afya ya Ardamata inayofadhiliwa na UNFPA huko El Geneina, Jimbo la Darfur Magharibi, Sudan.
© UNFPA Sudan
Mwanamke akipokea matibabu katika kliniki ya afya ya Ardamata inayofadhiliwa na UNFPA huko El Geneina, Jimbo la Darfur Magharibi, Sudan.

UNFPA ilivyorejesha matumaini ya wanawake na wasichana wa Darfur Magharibi Sudan

Afya

"Nilikuja kwenye kituo cha afya baada ya mapigano kutulia, lakini nilikuta kimeharibiwa hakukuwa na vitanda, vifaa, na mahitaji," anakumbuka Hiba, daktari katika mji wa El Geneina, katika Jimbo la Darfur Magharibi nchini Sudan. 

Kliniki ya Ardamata inaungwa mkono na shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA, na inapofanya kazi inatoa msaada muhimu kwa takriban watu 300,000, wote waliokimbia makazi yao ndani ya Sudan na kutoka jamii zinazowapokea. 

Huduma zake zinajumuisha msaada wa afya ya uzazi na jinsia, kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia na udhibiti wa kimatibabu wa ubakaji.

Licha ya ghasia na misukosuko iliyoenea tangu mzozo kuenea nchini Sudan mwezi Aprili 2023, wafanyakazi wa afya na misaada katika jamii wamejitolea kuendeleza kazi zao. 

Lakini wakati makundi yenye silaha yalipovamia na kupora kituo hicho mwezi Novemba, wafanyakazi hawakuweza tena kuhakikisha hata huduma za kimsingi, na kuacha pengo kubwa katika utoaji wa huduma kwa wale wanaohitaji zaidi.

Kuendelea kusambaza msaada

Kwa mujibu wa UNFPA mahali ambapo hali ya usalama iliruhusu, waliendelea kupeleka huduma moja kwa moja kwa wanawake, “baada ya kuharibiwa kwa kituo, tulitembelea wanawake wajawazito na wasichana majumbani mwao, hata hivyo, tulikabiliana na changamoto za upatikanaji na hatukuweza kushughulikia kesi ngumu,” ameelezea Sara, ambaye ni muuguzi na kuongeza kwamba  baadhi ya wanawake wajawazito, walilazimika kuwazalisha njiani.

Hali nchini Sudan ni mbaya, ambapo takriban watu milioni 6 ni wakimbizi wa ndani huku wengine milioni 4.5 kati yao wamekuwa wakimbizi wa ndani tangu Aprili ikiwa ni pamoja na wanawake wapatao 167,000 ambao kwa sasa ni wajawazito. 

Ripoti za unyanyasaji mkubwa wa kijinsia, kushurutishwa na usafirishaji haramu wa wanawake na wasichana unaongezeka kwa viwango vya kutisha, wakati mifumo ya ulinzi imefungwa na makazi ya muda yamezidiwa.

Katika kipindi cha mwaka mmoja, kumeripotiwa mashambulizi 60 kwenye miundombinu ya afya, na asilimia 70 ya vituo vya afya katika maeneo yenye migogoro havifanyi kazi, wahudumu wa afya hawajalipwa kwa miezi kadhaa na vituo vingi vimesalia bila watu, kuporwa au kuharibiwa,vituo vingi bado vimechukuliwa na vile vilivyobaki vinakabiliwa na upungufu wa damu, vifaa vya kutia kwenye mishipa, maji au drip na vifaa vya matibabu.

Mkunga katika kliniki ya Ardamata anamhudumia mwanamke mjamzito, mmoja wa takriban watu 167,000 waliokimbia makazi yao nchini Sudan kwa sasa.
© UNFPA Sudan
Mkunga katika kliniki ya Ardamata anamhudumia mwanamke mjamzito, mmoja wa takriban watu 167,000 waliokimbia makazi yao nchini Sudan kwa sasa.

Jibu la ustahimilivu

Baada ya kusaidia ukarabati wa kliniki mwezi Desemba 2023, UNFPA pamoja na mshirika wa ndani, Child Development Foundation, na wafadhili wa kimataifa walibadilisha vitu muhimu kama vile vitanda, taa, vifaa vya upasuaji na vifaa vya ukunga ili kliniki iweze kuendelea kutoa huduma.

"Tulizalisha watoto 49 katika kituo hicho mwezi Desemba, tunafurahi kuanza tena kuwahudumia wanawake na wasichana wa Ardamata." amesema mtoa huduma ya afya Khalid alipokuwa akizungumza na UNFPA. 

Ameongeza kuwa "Wanawake hawa wangeachwa bila huduma ya matibabu ikiwa kituo kingebaki bila huduma."

Wakati kliniki ikirejea kutoa msaada wake kamili, ikijumuisha afya ya uzazi na uzazi na kuzuia ukatili wa kijinsia, mfanyakazi wa afya Eman amesema, "sasa tunatoa huduma zote bila malipo, ikiwa ni pamoja na kujifungua na huduma baada ya kuzaa."

Ikifadhiliwa na Muungano wa Ulaya, Jamhuri ya Korea na Marekani, kliniki hiyo sio tu inatoa huduma ya matibabu, lakini pia inawapa wanawake na wasichana wa El Geneina hali ya usalama wakati huu ambao mzozo unaendelea nchini humo.

Uporaji na uharibifu ulilazimisha kliniki hiyo kusitisha kazi, huku wahudumu wa afya badala yake wakitoa huduma moja kwa moja kwa wanawake na wasichana majumbani mwao, wakati hali ya usalama inaruhusu.
© UNFPA Sudan

UNFPA nchini Sudan

UNFPA inasaidia vituo vya afya na maeneo salama yanayofanya kazi kote Sudan, pamoja na kliniki tisa za muda zilizotumwa kutoa huduma ya uzazi na ulinzi dhidi ya ukatili wa kijinsia katika majimbo ya Al Jazira, Blue Nile, Gedaref, Kassala, Kaskazini, Darfur Magharibi, na Nile White.

Afya na usalama wa wanawake na wasichana unahatarishwa hasa katika mazingira ya mizozo na ukimbizi, wanashurutishwa kutafuta hifadhi katika makazi yasiyo safi, yenye watu wengi na mara nyingi wanajikuta wakibeba jukumu la kukusanya chakula, kuni, na maji hivyo kuwaweka katika hatari ya ukatili na utekaji nyara kwani lazima wajitokeze peke yao.

UNFPA inasema wanawake na wasichana milioni 4.2 nchini Sudan wako katika hatari ya kufanyiwa ukatili wa kijinsia, idadi ambayo inaweza kuongezeka hadi milioni 6.9 mwaka wa 2024.

Licha ya kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa usalama, wafanyakazi wa kliniki ya Ardamata wanaendelea kujitolea kusaidia jamii zao maisha na ustawi wa mamilioni ya watu yanazidi kuning'inia kwenye mizani.