Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za haraka zichukuliwe kuhakikisha afya na usalama wa wanawake Darfur:UNFPA

UNFPA imekuwa ikiwasaidia wanawake wajawazito Darfur Magharibi kufuatia kuongezeka kwa ukosefu wa utulivu katika eneo hilo.
UNFPA
UNFPA imekuwa ikiwasaidia wanawake wajawazito Darfur Magharibi kufuatia kuongezeka kwa ukosefu wa utulivu katika eneo hilo.

Hatua za haraka zichukuliwe kuhakikisha afya na usalama wa wanawake Darfur:UNFPA

Amani na Usalama

Hali ya machafuko inayoendelea kwenye jimbo la Darfur Magharibi nchini Sudan imewaacha maelfu ya wanawake bila huduma za kutosha za afya ya uzazi na ulinzi na hivyo kutishia Maisha yao, afya na ulinzi wao imeonya ripoti iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UNFPA tangu tarehe 28 Desemba mwaka 2019 machafuko ya kikabila katika kambi ya wakimbizi wa ndani yamesababishwa kutawanywa kwa watu hao 40,000 ambao kati yako wanawake kwenye uwezo wa kuzaa wanakadiriwa kuwa 10,800.

Akifafanua Zaidi mwakilishi wa UNFPA nchini Sudan Massimo Diana amesema “Kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni kwenye kambi ya Darfur Magharibi , wanawake walilazimika kukimbia na kuacha nyumba zao zilizoteketezwa kwa moto na vitu vyao vyote. Mashambulizi hayo yaliwaathiri kisaikolojia na sasa wanahitaji msaada wa ushauri nasaha. Na kwa sababu hawana makazi binafsi wanaendelea kuhisi hawako salama na wako katika hatari kubwa ya kukabiliwa na machafuko na unyanyasaji.”

Kutokana na takwimu za wizara ya afya na maendeleo ya Sudan , UNFPA inasema kuna takriban wanawake wajawazito 3442 ambao wako katika hali mbaya wakihitaji huduma za afya ya uzazi. Na miongoni mwa wanawake hao walio wajawazito mia saba kati yao wana ujauzito wa miezi tisa bna wanatarajiwa kujifungua hivi karibuni katika makambi 41 ya wakimbizi wa ndani nchini humo. Hivyo shirika hilo linasisitiza kwamba hatua za haraka zinahitajika ili kuokoa Maisha na kuhakikisha wanawake hawa wanapata huduma za afya na usalama wao. Massimo Diana ameongeza kwamba “Kulegalega kwa huduma ya afya ya uzazi kwa wanawake wajawazito na ukosefu wa fursa za kujifungua salama ni sababu kubwa ya kupoteza Maisha kwa mama na Watoto wanaozaliwa. Pia kufurika kwa hospitali wakati huu ambao kuna tatizo la usalama ni suala la kawaida na kwa hali ya sasa Darfur Magharibi inamaanisha kwamba wanawake wanajifungua Watoto katika vyumba vilivyofurika na katika maeneo ya wazi.”

 

Msaada wa UNFPA na wadau

Katika siku 10 zilizopita pekee ripoti hiyo inasema watoto 373 wamezaliwa na hatua zimechukuliwa haraka kukabiliana na mahitaji ya lazima kwa ajili ya kujifungua salama na huduma za afya ya uzazi ikiwemo kupeleka wakunga 160.

Japo kuna hatua kiasi zilizopigwa lakini ripoti inasema idadi ya wakunga na maeneo salama ya kujifungulia bado ni changamoto na matokeo yake watu wanajifungua katika mahema  na maeneo mengine ikiwemo kwenye vyumba vya madarasa ambako kuna watu wengi wakiwemo wanawake wengine ambao sio wajawazito na watoto.

Kwa sasa UNFPA inaisaidia wizara ya afya ya Sudan na jumuiya ya chama cha msalaba mwekundu cha Sudan (SRCS) kuanzisha kliniki za afya ya uzazi katika makambi 31 ya wakimbizi wa ndani na kwa kupitia msaada huu kliniki hizo zitawekewa vifaa na tayari wakunga 60 wameshapelekwa kutoa huduma.

 

Mhudumu wa Afya kutoka Mongolia akitoa huduma kwa mama na mtoto Darfur,Sudan(10 Disemba 2012)
Picha/ UN/Albert Gonzales Farran
Mhudumu wa Afya kutoka Mongolia akitoa huduma kwa mama na mtoto Darfur,Sudan(10 Disemba 2012)

 

Kilichofanyika hadi sasa

UNFPA imeshasafirisha vikasha 31 vyenye vifaa tofauti vya huduma ya dharura ya uzazi kwenye eneo la El Geneina, na pia vifaa kadhaa vya usafi binafsi vimewasili. Vifaa hivyo vimesafirishwa kutoka mji mkuu Kharthoum hadi El Geneina, vikitarajiwa kusaidia kukidhi mahitaji ya wanawake wote wajawazito.

Diana mwakilishi wa UNFPA Sudan anasema “Kukosa huduma za msingi za afya ya uzazi kukasababisha kuongezeka kwa idadi ya vifo vya kina mama na Watoto wakati wa kujifungua hivyo hatua hii ni ya kuokoa maisha .”

Ameongeza kuwa ongezeko la watu kutawanywa linaongeza pia hatari ya ukatili wa kijinsia hususan kwa wanawake na wasichana ambao sasa wanahitaji fursa ya huduma ya waliopitia ukatili wa kijinsia. “Ukatili wa kijinsia ni moja ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu duniani , vipaumbele vyote kuhusu suala hili ni lazima vipewe uzito wa juu na kwa haraka bila kujali kama ni dharura ama la.”

Mama huyu kutoka kambi ya Kassab Kutub Darfur ya kaskazini ahuzunishwa  na visa vya ubakaji katika eneo hilo.
Photo: UNAMID/Albert González Farran
Mama huyu kutoka kambi ya Kassab Kutub Darfur ya kaskazini ahuzunishwa na visa vya ubakaji katika eneo hilo.

 

Taarifa za kuaminika ikiwemo tathimini ya haraka inaashirika kuwa ukatili wa kijinsia (GBV) kwenye makambi ya wakimbizi wa ndani umekuwa ukifanyika kwa kiasi kikubwa na katika mifumo tofauti.

Na ili kukabiliana nao hatua zinaimarishwa kuzuia na kuudhibiti ukatili huo ikiwemo kuratibu na kutoa msaada wa kisaikolojia na huduma zingine za msingi kwa waathirika.

Huduma za afya za kuokoa maisha

Ili kukidhi mahitaji ya kukabiliana na hali mbaya ya afya na huduma za ulinzi, timu ya waratibu wa masuala ya ukatili wa kijinsia na afya ya uzazi wamepelekwa El Geneina na vifaa vya dharura vya huduma ya afya ya uzazi vimeshatumwa kusaidia wanaohitaji. "UNFPA imegawa vifaa vya kusaidia wakati wa kujifungua kwa kina mama na  na kwenye vituo vya afya ili kuhakikisha usafi na mazingira salama wakati wa kujifungua. Na hatua hizo ni za kuokoa maisha kwa wote mama na mtoto.”