WHO yasaidia mahitaji ya dharura ya afya kwa walioathirika na machafuko Darfur

14 Januari 2020

Shirika la afya duniani WHO na wadau wengine wa afya wanashirikiana kuchukua hatua kukabiliana na mahitaji ya kiafya ya watu walioathirika na machafuko huko El Geneina, Darfur Magharibi nchini Sudan.

Hadi kufikia leo WHO imeshafikisha msaada wa madawa na vifaa vingine vya tiba 120 kwa watu 200 wakiwemo wanaohitaji huduma za dharura au upasuaji.

Vitu vingine vilivyofikishwa na wadau wengine wa afya ni pamoja na dawa za kutibu magonjwa ya kuhara, maradhi yanayosumbua watoto wadogo na vifaa vya kusaidia kina mama wakati wa kujifungua.

Kwa mujibu wa Dkt. Hoda Atta kaimu mwakilishi wa WHO nchini Sudan “Kutokana na mazingira ya watu kufurika wanakoishi na uhaba wa huduma za maji salama na usafi hatari ya kusambaa kwa maradhi ya kuambukiza yatokanayo na maji ni kubwa. Hivyo ufuatiliaji wa magonjwa umeanzishwa ingawa bado kuna pengo kubwa katika chanjo ambalo linahitaji kushughulikiwa haraka.”

Machafuko baina ya makabila kinzani kwenye eneo hilo yamesababisha makumi ya watu kuuawa na mamia kujeruhiwa , huku wengine zaidi ya 70,000 wanaoishi makambini na katika vijiji vya jirani wakiathirika.

Hali halisi

Mhudumu wa afya kwenye hospitali ya El Geneina alishambuliwa na watu wenye silaha na hospital hiyo iliacha kutumika kwa muda kutokana na kutokuwa na usalama.

Kuanzia Januari 10 mwaka huu watu wanaofungasha virago na kukimbia mji wa Geneina wanaendelea kusaka hifadhi mashuleni na kwenye maeneo mengine ya mikusanyiko ambako kuna ripoti za upungufu wa chakula , maji salama, vyoo na malazi yanayostahili.

Kwa sasa hivi vituo saba vya huduma za afya vimeanzishwa na wadau wa afya ili kuhudumia maeneo ambako wapo watu waliotawanywa na machafuko na wale wanaohitaji huduma za hospitali wanapelekwa katika hospitali ya mafunzo ya Geneina. Magari mawili ya kubeba wagonjwa ndio yanayowasafirisha wagonjwa hao na kubeba vipimo vya maabara kwa ajili ya kufanyika uchunguzi hoospitali.

“WHO na washirika wake wa afya wako katika tahadhari ya hali ya juu wakati  huu tukikabiliana na mahitaji ya watu wote walioathirika na wakati huohuo tukifanya kila liwezekanalo kuepuka uwezekano wa hatari kubwa ya kiafya”  ameongeza Dkt. Atta.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud